Serikali yapiga jeki kiwanda cha vijana, wanawake

SHINYANGA: SERIKALI imetoa zaidi ya Sh milioni 95.6 kwaajili ya kiwanda kidogo cha vijana na wanawake kilichopo kitongoji cha Kalangale Kata ya Kiloleli Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kwaajili ya kutengeneza bidhaa za ngozi.
Kiwanda hicho kilianza rasmi mwaka 2021 ambapo bidhaa zinazotengenezwa kutokana na kuchakatwa kwa mazao ya ngozi ya ngo’mbe na mbuzi ni viatu,mikanda na mikoba.
Hayo yamesemwa leo na Katibu msaidizi wa vituo vya taarifa na maarifa vilivyojengewa uwezo wa kuibua na Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) Kata ya Kiloleli Zacharia Pimbi walipokuwa wakitoa taarifa kwa waandishi wa habari ambapo alisema halmashauri pia iliwakopesha bila riba Sh milioni 10 mwaka 2023 kwaajili ya kuendesha kiwanda hicho.
Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kupitia mradi wa mabadiliko ya tabia ya nchi (EBBAR) ulitoa fedha hizo na zaidi ya Sh milioni 5 zilitumika kwaajili ya kuwajengea uwezo wanakikundi ambao wanaendesha kiwanda hicho.
Makamu Mwenykiti wa kikundi hicho, Regina Nyahigi amesema wameungana vikundi viwili vya vijana na wanawake ambapo imewasaidia kujinyanyua kiuchumi baada ya bidhaa za viatu,mikoba na mikanda kutengenezwa na kwenda kwenye kila maadhimisho au Magulio kuuza na fedha kuweka benki.



