Serikali yatangaza mikakati kuwalinda wanafunzi

DODOMA: SERIKALI imeeleza kuwa usalama wa wanafunzi ni kipaumbele chake kikubwa ambapo mikakati mbalimbali imekua ikitekelezwa ili kuhakikisha wanafunzi wanakuwa katika mazingira salama mashuleni.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 22, bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Zainabu Katimba wakati wa kipindi cha maswali na majibu ambapo Mbunge wa Viti Maalum, Latifa Juakali alihoji mpango wa serikali katika kuwalinda wanafunzi mashuleni alijibu swali hilo Naibu Waziri amesema baadhi ya mikakati inayotumika kuwalinda wanafunzi ni kampeni za kupinga ukatili wa kijinsia kuanzia nyumbani, njiani na shuleni kwa kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama.
“Mafunzo kuhusu shule salama kwa wadau muhimu wa ulinzi na usalama wa wanafunzi ambapo mwaka 2024/25 yameendeshwa mafunzo kwa walimu 7,451 wa ushauri na unasihi, wakuu wa shule za msingi 17,817, maofisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata 900, wenyeviti wa kamati za shule 1,980 na wenyeviti wa bodi za shule 580” amesema Katimba
Pia ameeleza mikakati mingine ni kuanzisha dawati la ulinzi na usalama wa mtoto. Aidha ameongeza kuwa ngazi ya Kijiji na Mitaa yameanzishwa mabaraza ya watoto yanayojumuisha wanafunzi wa msingi na sekondari na watoto waliopo kwenye mfumo usio rasmi.
Katika hatau nyingine Naibu Waziri huyo wa TAMISEMI amesema Serikali itaendelea kufanya tathmini ya kina kuhusu changamoto zinazowakabili wanafunzi shuleni, njiani na nyumbani ili kuboresha mikakati kuzitatua.