Serikali yawakumbuka watoto wenye uhitaji Mtwara

SERIKALI mkoani Mtwara kwa kushirikiana na wadau mbalimali imekabidhi misaada mbalimbali kwa watoto zaidi ya 1,000 wenye mahitaji maalumu mkoani humo uliyogharimu Sh milioni 8.
Akizungumza leo wakati wa ghafla fupi ya kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patric Sawala amesema anaamini moyo huo wa kuweza kuwashika mkono watoto wao utaendelea ili waendelee kupata faraja zaidi.
‘’Niwashukuru wadau wote ambao wameweza kushiriki kwa namna moja ama nyingine tunaamini moyo huu wa kuweza kuwashika mkono watoto wetu utaendelea ili watoto wetu wa wenyewe waendelee kupata faraja zaidi,’’amesema Sawala.

Hata hivyo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa na upendo wa kuweza kushiriki na makundai mbalimbali katika nyakati mbalimbali ikiwemo sikuu za mwisho wa mwaka.
‘’Mheshimiwa Rais ameonyesha njia ya namna na kushrikiana na kuwapa nafasi watoto wetu ambao wana mahitaji maalum waliyopo kwenye vituo ambao nao wanahitaji faraja kama wengine katika sikuu hizi za mwisho wa mwaka, niwashukuru sana waratibu kwa kuweza na sisi kama mkoa kuona ni namna gani tunaenda kuunga mkono jitihada hizi’’
Mwalimu na Mlezi kutoka Kituo cha kulelea watoto cha Upendo Rehabilitation Center kilichopo magomeni Manispaa ya Mtwara Mikindani, Sikudhani Ayubu amempongeza mkuu huyo wa mkoa kwa kuwapatia msaada huo na utu aliyouonyesha kwa watoto hao.

Mmoja wa watoto hao wenye wahitaji maalum akiwemo Nurdini Abdallah kutoka kituo cha Rahaleo Manispaa hiyo ameushukuru uongozi wa mkoa huo kwa kuendelea kuwajali kwasababu mara nyingi wamekuwa wakipatiwa msaada hivyo wanakuwa ni watu wenye faraja wakati wote.
Aidha, watoto hao waliyopatiwa msaada huo ni kutoka kwenye vituo sita kutoka katika baadhi ya halmashauri mkoani humo ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.



