Serilkali yatoa Bil 9/- kuwezesha ujuzi, nguvu kazi

SERIKALI imetoa Sh bilioni 9 kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa ajili ya kuwezesha nguvukazi ya taifa kupata ujuzi stahiki unaoendana na ushindani katika soko la ajira.
Fedha hizo zimetolewa kupitia Programu ya Taifa kukuza ujuzi ambayo imejikita katika mafunzo ya uanagenzi, kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi, mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi kwa wahitimu na mafunzo ya kukuza ujuzi kwa walio makazini.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Daudi Silasi amesema hayo wakati akifunga mafunzo kwa vitendo kwa wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita.
Amesema serikali imejipanga kuhakikisha wachimbaji wadogo wanakuwa sehemu ya maendeleo ya taifa kwa kuwajengea uwezo endelevu kupitia na kuwahusisha kwenye mnyororo mzima wa thamani ya madini.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji, Neema John amesema mafunzo hayo yamewasaidia kujitambua kama wadau muhimu katika sekta ya madini na kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
“Tulikuwa tunafanya kazi kwa mazoea bila kujua athari za kiafya wala mazingira, sasa tunajua umuhimu wa kutumia vifaa sahihi, kuchimba kwa mpangilio na kuhifadhi mazingira”, amesema Neema.
Naye, Emmanuel Kapunda, amesema mafunzo hayo yamewafungua macho kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya madini, hasa kwa wachimbaji wadogo ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikumbwa na changamoto ya ukosefu wa elimu ya biashara na usimamizi wa rasilimali.
Mafunzo hayo, yameendeshwa kwa nadharia na vitendo ili kuwajengea uwezo wachimbaji kuhusu uchimbaji salama, uhifadhi wa mazingira, matumizi ya teknolojia, usalama kazini na masuala ya kisheria na masoko ya madini.