Sh bilioni 9 kukamilisha ofisi ya RC Kagera

KAGERA: Serikali mkoani Kagera imesaini mkataba na mkandarasi wa ujenzi wa jengo la ofisi mpya ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera litakalojengwa kwa Sh bilioni 9  awamu mbili.

Aidha, awamu ya kwanza itagharimu Sh bilioni 4.6 kwa kujengwa na mkandarasi M/s Skywards Construction Company Limited wa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kumkabidhi mkandarasi eneo la ujenzi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amesema kwa sasa ni muhimu Mkoa wa Kagera kuwa na ofisi ya kisasa yenye vifaa vya kisasa vinavyoendana na sayansi na teknolojia ili kutoa huduma nzuri na zenye uhakika kwa wananchi.

RC Mwassa amesema kuwa ofisi ya sasa imepitwa na wakati kwani ilijengwa miaka ya 1960 lakini eneo ilipo ofisi kuna changamoto ya maji kujaa kutoka Ziwa Victoria jambo ambalo linapelekea eneo hilo kuwa hatarishi kadri ya siku zinavyosogea kutokana na mabdiriko ya tabia nchi na kutoruhusu ujenzi kufanyika katika eno hilo.

“Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera inazaidi ya miaka 60 kuendelea kudumbukiza pesa pale kwa kufanya marekebisho ni Matumizi mabaya ya fedha za serikali ,kwa sasa tunahitaji kujenga ofisi nzuri yenye mifumo ya kisasa lakini jengo ambalo litakuwa moja ya majengo ya kitalii wa Mkoa wa Kagera,” amesema Mwassa.

Amesema licha ya Mkoa wa Kagera kupakana na nchi nyingi za Afrika Mashariki bado kumekuwepo na changamoto ya kukosa eneo la kukaribisha wageni hivyo anaamini miongoni mwa sifa za jengo jipya ni kuwa na sehemu nzuri ya kukaribisha wageni.

Mkadarasi M/s Skywards Construction Company Limited ameelekezwa kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa jengo la ofisi kwa awamu ya kwanza kulingana na mkataba ndani ya miezi 12.

Huku , Mshauri elekezi M/s Goztecture Group naye amesisitizwa kufanya kazi yake kwa ufanisi ya kumsimamia na kumshauri Mkandarasi ili mradi huo uweze kujengwa kwa viwango kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali.

Gozibert Kakiziba Mkurugenzi wa Kampuni ya M/s Goztecture (Mshauri Elekezi) wa mradi amesema katika hafla hiyo kuwa mchoro wa jengo jipya la ofisi ya mkuu wa mkoa umezingatia mambo muhimu manne ambayo ni uimara wa jengo litadumu zaidi ya miaka 100, uzuri wa jengo kuwavutia wananchi na wawekezaji, uoto wa asili kutunzwa ili mandhari iendelee kuvutia, pia jengo hilo litazingatia utawala au mamlaka kwenye usanifu wake.

Mhandisi Raphael Nyatega, Mhandisi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa Kagera amesema faida za utekelezwaji wa mradi huo ni kuboresha utoaji wa huduma nzuri kwa wananchi, kuboresha utendaji kazi kwa watumishi, kuvuti na wawekezaji kwa kuwa mkoa wa Kagera upo katika eneo la kimkakati na mwisho kuboresha mandhari ya mji wa Manispaa ya Bukoba.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera inajengwa katika viwanja vya Serikali vilivyopo Kata ya Rwamishenye Manispaa ya Bukoba, ofisi ya sasa ya Mkuu wa Mkoa Kagera ipo Kata Miembeni karibu na fukwe za Ziwa Victoria Manispaa ya Bukoba.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button