Sh milioni 403 kurejesha Mawasiliano Mbinga

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Mbinga umepokea jumla ya shilingi milioni 403.7 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kurejesha mawasiliano ya barabara zilizoharibiwa na mvua za masika pamoja na tetemeko la ardhi lililotokea mwezi Mei 2024.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbinga, Mhandisi Oscar Mussa, amesema fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi miwili mikubwa ya ukarabati wa barabara muhimu kwa wananchi wa maeneo husika. SOMA: Sh bilioni 50 kuimarisha miundombinu ya mawasiliano

“Katika kipindi cha masika tulikumbwa na madhara makubwa yaliyosababisha kuporomoka kwa udongo na kuharibu miundombinu ya barabara. Serikali ilitupatia shilingi milioni 283.2 kwa ajili ya kurudisha mawasiliano katika barabara ya Langilo–Mkoha,” alisema Mhandisi Mussa.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 7.2 inahudumia wakazi wa Kata ya Langilo, hasa Kijiji cha Mkoha, ambapo madhara makubwa yalijitokeza katika eneo la daraja la Mto Makomba kutokana na udongo kuporomoka na mawe kuanguka barabarani.

Mhandisi Mussa amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza Machi 2024 na unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu, huku kazi zilizokamilika zikijumuisha kurudisha tuta, kujenga mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa zaidi ya kilomita moja, na kuondoa mawe yaliyokuwa yameziba barabara.

Aidha, alitaja mradi wa pili kuwa ni ukarabati wa barabara ya Longa–Kipololo–Litoho, iliyopokea shilingi milioni 120.6 baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhi. “Eneo la Kalavati, katika Mto Ntunduwalo, liliporomoka tuta, lakini kwa sasa barabara hiyo imefunguliwa na inapitika kwa usalama,” alisisitiza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button