Sheria makosa ya uhujumu uchumi kurekebishwa

DODOMA; BUNGE mchana huu limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2025, huku miongoni mwa sheria zinazotarajiwa kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200.

Akiwasilisha muswada huo bungeni mapema leo Juni 5, 2025, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amesema katika sura hiyo wanapendekeza kufutwa kwa kifungu cha 26.

“Sehemu ya Pili ya Muswada inapendekeza marekebisho katika Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200, ambapo kifungu cha 26 kinapendekezwa kufutwa.

“Marekebisho haya yanakusudia kuwezesha mashtaka chini ya Sheria hii kufunguliwa bila kuhitaji ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka.

“Takwa la ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka kabla ya kufungua shtaka chini ya Sheria hii liliwekwa miaka ya nyuma, ambapo sehemu kubwa ya mashtaka yalikuwa yanaendeshwa na askari polisi kwa kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka haikuwa imeenea katika mikoa na wilaya zote nchini.

“Hivyo, kulikuwa na umuhimu wa kupata ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka ili kudhibiti ufunguaji holela wa mashtaka.

“Katika mazingira ya sasa ambapo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefungua ofisi zake hadi ngazi ya Wilaya na kesi zote za jinai zinaendeshwa na Mawakili wa Serikali wanaowajibika moja kwa moja kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, masharti ya kupata ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka yanakosa mantiki ya kuendelea kuwepo na yanaweza kuchangia ucheleweshaji wa haki jinai,” amesema Mwanasheria Mkuu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button