Shirika lafafanua linavyokuza sekta ya maziwa

MOROGORO: Shirika la Heifer International Tanzania limeendelea kuonesha mafanikio yake katika kubadilisha sekta ya maziwa nchini, kwa kipaumbele maalum katika kuwawezesha wanawake na vijana pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa.

Katika maadhimisho hayo ya 28 ya wiki ya kimataifa ya maziwa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo, Abdul Mhinte alikuwa mgeni wa siku ya leo ya mwisho ya maonesho ambapo alitembelea mabanda na kutambua mchango wa wadau kwenye sekta ya maziwa.

Maonyesho hayo yaliyoanza Mei 27 yanatarajia kutamatishwa Juni 1, 2025.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika mkoani Morogoro, Mhinte alilipongeza shirika hilo kwa mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya maziwa na kusisitiza umuhimu wa mashirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo.

“Shirika la Heifer limeonesha mfano wa kuigwa katika kuleta maendeleo ya kweli kwa wafugaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya maziwa nchini. Tunathamini mchango wao na tunaendelea kushirikiana kwa karibu,” alisema.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Heifer International, Nyamate Musobi, alisema shirika hilo limekuwa mstari wa mbele katika kuleta mageuzi chanya kwenye sekta ya maziwa kupitia miradi jumuishi na ya kijamii.

“Tumejikita katika kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika uzalishaji wa maziwa na kuongeza tija kwa kutumia mbinu bora za kisasa. Lengo letu ni kujenga mnyororo thabiti wa thamani ambao unawanufaisha wafugaji na jamii kwa ujumla,” alisema Musobi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button