‘Sido inatoa mafunzo ya vifungashio wajasiriamali’

DODOMA; SHIRIKA la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), linatekeleza mkakati wa mafunzo ya ufungashaji wa bidhaa kwa wajasiriamali. Bunge limeelezwa.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe ametoa kauli hiyo bungeni leo Juni 6, 2025 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Tamima Haji Abass aliyehoji mkakati wa serikali kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo ili kuwawezesha kuwa na vifungashio bora vya bidhaa zao.
“Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) inatekeleza mkakati wa mafunzo ya ufungashaji wa bidhaa kwa wajasiriamali ikiwemo namna ya kutengeneza vifungashio, kutumia chapa (brand) na lebo.
“Vilevile, SIDO inatoa elimu kwa waundaji (Designers) na wachapaji wa lebo za bidhaa ili kuwaongezea ujuzi katika kuwahudumia wajasiriamali. Lengo la mafunzo hayo ni kuboresha vifungashio vya bidhaa za wajasiriamali ili ziweze kushindana sokoni.
“Aidha, SIDO hununua vifungashio kwa jumla (Bulk Procurement) kutoka nje ya nchi na kuviuza kwa rejareja na kwa bei nafuu katika ofisi za SIDO za mikoa kwa wajasiriamali. Hatua hiyo huwawezesha wajasiriamali kupata vifungashio bora na kwa bei nafuu,” amesema Naibu Waziri.