Sirro ahimiza nishati safi vijijini

KIGOMA: Mkuu wa Mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro amezitaka kampuni zinazosambaza nishati safi ya kupikia kuhakikisha nishati hiyo inafikishwa vijijini kwa wananchi ili waweze kuitumia.

Balozi Sirro alisema hayo wakati uongozi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na viongozi wa kampuni ya Envotec Services Ltd walipofika ofisini kwake kutoa taarifa ya kampuni hiyo kuuza na kusambaza majiko banifu kwa gharama nafuu mkoani Kigoma.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa majiko banifu na nishati safi ya kupikia yamekuwa na matokeo chanya katika kukabili uharibifu wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya ya tabia nchi hivyo wananchi hawana budi kumuunga mkono Rais Samia katika mpango wa matumizi ya nishati safi na salama.

Akiwasilisha taarifa ya mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa Kigoma, Mhandisi wa miradi kutoka REA, Raya Majallah alisema kuwa Katika kufanikisha hilo REA imekuja na mpango wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku ambapo mkoa Kigoma unatarajia kupata majiko 8424 kila wilaya ikipata majiko 1404 katika wilaya sita za mkoa huo.

Mhandisi huyo wa miradi REA alisema kuwa gharama ya jiko moja ni Sh 50,990 lakini serikali imetoa ruzuku ya asilimia 85 sawa na Sh 43,341 na hivyo mwananchi atalazimika kununua jiko kwa Sh 7,649.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button