Slovakia yafungua Ubalozi Tanzania

BALOZI Mteule wa kwanza wa Slovakia nchini Tanzania, Ivan Lančarič amewasilisha nakala za Hati za Utambulisho kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe jijini Dodoma.
Lančarič amewasilisha nakala hizo za Hati za Utambulisho kufuatia nchi yake kufungua Ubalozi nchini Mwezi Desemba 2025.

Akipokea Nakala za Hati hizo, Dk Maghembe amesema ufunguzi wa Ubalozi huo ni matokeo ya utekelezaji uliotukuka wa Diplomasia ya Tanzania duniani, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Ubalozi huu utakuwa kichocheo cha kukuza ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Slovakia, hususan katika nyanja za uwekezaji, biashara na utalii,” Dk Maghembe amesema.

Kwa upande wake, Lančarič alieleza ufunguzi wa ubalozi mpya nchini Tanzania ni utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, ambayo inalenga kutanua wigo wa uwakilishi barani Afrika.
Amesema Ubalozi huo utawakilisha sio tu Tanzania bali nchi nyingine za Afrika kama vile Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Congo Brazzaville, Burundi, Gabon, Cameroon na Guinea ya Ikweta.



