State Oil yachangia Sh Mil 500 harambee CCM

DAR ES SALAAM; Kampuni ya Usafirishaji wa Mafuta nchini ya State Oil, imechangia Sh milioni 500 katika harambee ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuchangisha  fedha kwa ajili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Harambee hiyo ya kitaifa ilifanyika Dar es Salaam jana na zilichangwa zaidi ya Sh bilioni 86, kati ya fedha hizo, Sh bilioni 56.3 ni fedha taslimu na Sh bilioni 30 ni ahadi.

Mwenyekiti wa bodi wa kampuni hiyo, Nilesh Suchak  amesema wameamua kuchangia fedha hizo  kutokana na kuvutiwa na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni Rais wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi wa nchi.

Baadhi ya waliochangia ni Rais Samia (Sh milioni 100), CCM upande wa Zanzibar ulitangaza kukusanya Sh bilioni nne, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema anachangia Sh milioni 50 na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira alichangia Sh milioni 20.

Wengine waliosimama na kutaja mchango (Shilingi) ni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango (milioni 20), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (milioni 20), Makamu wa Pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah alisema anachangia Sh milioni 20, Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson anachangia Sh 20.

Dk Tulia alisema Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zuberi Ali Maulid anachangia Sh milioni 20. Wachimbaji walitangaza kuchangia Sh bilioni 16.2 na kampuni ya GSM imechangia Sh bilioni 10 na taasisi mbalimbali pamoja na wafanyabiashara nao walichangia.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button