SUA yapata miradi 36 yenye thamani Bil.10.5

CHUO  Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA ) kimeeleza kuwa hadi kufikia Oktoba mwaka huu  miradi mipya ya utafiti 36 yenye thamani ya sh bilioni 10.5 imepatikana. Kati ya miradi hiyo 10 inafadhiliwa na wafadhili wa nje, miradi miwili ya Serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na miradi 24 inafadhiliwa na Chuo Kikuu hicho kupitia mapato yake ya ndani.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu hicho,  Andrew Massawe amesema hayo kabla ya kumkaribisha mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mstaafu na Waziri Mkuu Mstaafu , Joseph Warioba  wakati wa mahafali ya 46 ya Chuo Kikuu hicho yaliyofanyika Kampasi ya Edward Moringe mkoani Morogoro.

Massawe amesema tafiti hizo zimeendelea kuchangia katika kukuza maarifa na kutatua changamoto katika sekta za kilimo, mifugo , mazingira na maendeleo ya jamii. Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu hicho amesema  baraza linaendelea kusimamia mikakati ya kuimarisha vyanzo mbadala vya mapato  ya ndani kuoitia miradi ya kibiashara , ushauri wa kitaaluma na uwekezaji katika maeneo ya kimkakati.

Amesema katika kutekeleza jukumu la usimamizi wa shughuli za utafiti, baraza linaendelea kuhimiza matumizi ya matokeo ya kitafiti zinazofanywa chuoni kuchangia katika sera na mipango ya maendeleo ya Taifa. Massawe pia amesema baraza hilo linasimamia kwa karibu shughuli za ugani na ushauri unaotolewa na Chuo Kikuu hicho kwa wadau mbalimbali hususani katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi , mazingira  na maendeleo vijijini.

Amesema  hadi sasa wadau 79,147 wamenufaika na huduma hiyo wakiwemo wakulima , wafugaji, watafiti , maofisa ugani na watumishi  kutoka sekta binaafsi na sekta za umma ambapo asilimia 48 ya wanufaika walikuwa ni wanawake. SOMA: SUA yazindua mitaala mipya masomo elimu ya amali

Kwa upande wake  Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Raphael Chibunda amesema katika mahafali  hayo jumla ya wahitimu ni 3,560 wakiwemo wanaume 2,029 na wanawake 1,531. “ Kwa kawaida kuhitimu katika Chuo Kikuu SUA haijawahi kuwa lele mama , na kwa dhati ya moyo wangu ninayofuraha kuwapongeza wahitimu wote “ amesema Profesa Chibunda.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho alitaja wahitimu wa shahada ya kwanza walikuwa  3,275 kati yao wanaume 1,861 na wanawame 1,413, shahada za umahili 127 kati yao wanaume 76 na wanawake 51. Profesa Chibunda alitaja wahitimu mwengine 18 walikuwa ni wa shahada uzamivu (PhD) na kati yao wanaume 12 na wanawake sita , wahitimu wa stashahada 100  na wahitimu wa Astashahada 38.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho amesema katika mahafali hayo wanawake ni 1,531 ambao ni sawa na asilimia 42.95 ya wahitimu wote .Akizungumza baada mahafali hayo, Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu hicho (2025/ 2026), Shahidu Iddy aliwaasa wahitimu hao kutumia elimu yao, ujuzi  na maarifa yao kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii kupitia taaluma waliyonayo na waliyoipata  kutoka SUA .

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button