CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimefanikiwa kupata miradi mipya ya utafiti 11 yenye thamani ya Sh bilioni 4.5 katika kipindi cha mwezi Mei hadi Oktoba mwaka huu.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Raphael Chibunda amesema hayo katika mahafali ya 44 yaliyofanyika Kampasi ya Edward Moringe na kuhudhuliwa na wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa vyuo pamoja na balozi wa Msumbiji nchini.
Mahafali hayo ya 44 yalijumuisha wahitimu 3,061, kati yao wanaume 1,650 sawa na asilimia 53.9 na wanawake 1,411 ambao ni sawa na asilimia 46.1.
Profesa Chibunda licha ya kupata miradi hiyo, chuo hicho kimeendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kutekeleza programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) (Bulding Better Tomorrow) hasa katika kutafuta vijana wa kupata ajira ya muda na endelevu.
“SUA tulipewa jukumu la kusaili na kujaza nafasi 2,000 za wagani wa zao la pamba baada ya usaili wa awamu ya tatu chuo kimeweza kupata wagani 700 na usaili wa awamu ya nne utaendelea hivi karibuni,” amesema Profesa Chibunda.
“Kupitia program hii wahitimu wetu wa Shahada ya Kilimo na Vipando karibu wote wanauhakika wakupata kazi na hata wahitimu wa leo baadhi yao wamefanya usaili na kufaulu,” amesema Chibunda.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa nafasi hiyo kwa wahitimu wa Chuo Kikuu SUA.
Profesa Chibunda amesema chuo pia kimeendelea kuboresha mitaala yake ili kutoa mafunzo yanayolenga kumjengea mwanafunzi ujuzi, weledi na stadi za kujiajiri na kujirika ikiwa na kuwaongezea fursa za kujenga ubunifu na kukuza stadi kazi zinazozingatia viwango vya kimataifa.
Mwenyekiti wa Baraza la SUA ,Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman amesema kuwa baraza hilo liliidhinisha mapitio wa mpango wa miaka 10 kuanzia mwaka 2024 hadi 2034.
Amesema baraza limeendelea kuhimiza chuo kutilia mkazo zaidi katika mafunzo kwa vitendo kwa kuboresha mashamba darasa,karakana za uhandisi,maabara za mafunzo ya misitu ili kutoa fursa kwa wanafunzi na wadau wengine kupata mafunzo kwa vitendo ili waweze kuongeza maarifa.
Nao baadhi ya wahitimu kwa nyakati tofauti wamesema wanayofuraha ya kutumiza ndoto zao na walichokipata wakiwa chuoni kitawasaidia kujiajiri wao wenyewe wakiwa ndani ya nchi na hata nje ya nchi .
“ Binafsi elimu niliyoopata hapa SUA ni ya kiwango cha juu ina mifumo yote ambayo inamwezesha mhitimu kuweza kujiajiri ama kuajirika popote pale duniani “ amesema Vicent Alfred.