SUA yazindua mitaala mipya masomo elimu ya amali

MOROGORO: CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanzisha mitaala mipya sita ya Ualimu wa Amali inayolenga kuinua ubora wa elimu na kukidhi mahitaji ya walimu kufuatia mabadiliko makubwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Mitaala mipya hiyo inalenga kuwaandaa walimu wa kufundisha masomo ya amali ili kukidhi mahitaji katika shule za msingi na sekondari kwa ajili ya kuandaa vijana kushiriki kikamilifu kwenye maendeleo ya jamii na uchumi wa taifa.

Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda alisema kuwa mitaala hiyo mipya imeundwa kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha taifa linapata walimu stadi watakaoendana na mabadiliko ya mfumo wa elimu unaolenga kutoa maarifa na ujuzi kwa vitendo unaolenga kujiajiri.

“SUA imeanzisha mitaala mipya sita inayojibu mahitaji ya mabadiliko ya elimu nchini, hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha tunaandaa walimu mahiri wa kufundisha masomo ya amali kwenye shule zetu,” amesema Profesa Chibunda.

Profesa Chibunda amesema mitaala hiyo mipya imeshaidhinishwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kwamba Chuo Kikuu hicho inakuwa cha kwanza kutekeleza maagizo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya kuandaa mitaala na kufundisha walimu wa masomo ya amali.

Amesema hatua hiyo ni baada ya kubainika kwa changamoto kubwa ya uhaba wa walimu wenye sifa na ujuzi wa kufundisha masomo ya elimu ya amali nchini .

Profesa Chibunda ametaja mitaala mipya hiyo inayoanza kutumia mwaka huu wa masomo ni Shahada ya Ufundishaji wa Uzalishaji wa Mazao ya Kilimo, Shahada ya Ufundishaji wa Ushonaji na Mitindo ya Mavazi na Shahada ya Ufundishaji wa Bustani na Mboga .

Shahada nyingine ni Ufundishaji wa Lishe na Huduma ya Chakula, Shahada ya Ufundishaji wa Ufugaji wa Viumbe wa Majini, pamoja na Shahada ya Ufundishaji wa Uzalishaji wa Mifugo.

Profesa Chibunda amesema mitaala hiyo inalenga kujenga uwezo wa walimu kufundisha stadi za maisha shuleni na kuandaa kizazi cha vijana wabunifu na wachapa kazi watakaoweza kujiriwa na kujiajiri.

Amesema walimu watakaopitia mafunzo hayo wataweza kupeleka mabadiliko shuleni kwa kufundisha kilimo, lishe, ushonaji, bustani na ufugaji wa viumbe maji yakilenga kuwandaa wanafunzi kwa maisha halisi ya kujitegemea .

“ Mitaala hii ni matokeo ya tafiti na mijadala ya kina kuhusu kile ambacho elimu inapaswa kutoa ili kukidhi matarajio ya taifa , elimu yenye tija, ubunifu na inayojibu changamoto za kitaifa, amesema Profesa Chibunda.

Profesa Chibunda amesema Mitaala hiyo mipya inalenga kuunganisha elimu na ujuzi wa moja kwa moja unaohitajika sokoni, na hivyo kutoa suluhisho kwa matatizo ya ajira na maendeleo duni ya jamii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button