Sumaye amsifu Dk Samia

SIHA, Kilimanjaro: WAZIRI Mkuu Mstaafu na Mratibu wa Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanda ya Kaskazini, Fredrick Sumaye amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania ndani na nje ya mipaka kwa namna anavyoongoza serikali na kuipa heshima nchi kimataifa.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Siha, Kilimanjaro juzi Sumaye alisema Watanzania wanapaswa kujivunia kwa kuwa na kiongozi mwenye heshima kubwa duniani, kwani katika kipindi cha miaka mitano ya urais wake amejipambanua kama kiongozi shupavu na asiyechoka.
“Najua tunamfahamu sana mama Samia, picha zake tunaziona, hotuba zake tunazisikiliza, lakini kuna mambo ya ziada ambayo pengine wengi hawayafahamu. Mama Samia amekuwa mchapa kazi asiyechoka. Katika mizunguko ya kampeni kila siku utaona kama ni mpya, akichapa kazi kama alivyokuwa akiongoza nchi na chama chetu,” alisema Sumaye.
Aliongeza kuwa heshima ya Rais Samia kimataifa imeiwezesha Tanzania kualikwa kwenye mikutano mikubwa ya dunia ikiwemo ile ya nchi tajiri 20 (G20), jambo ambalo kwa kawaida si rahisi kwa viongozi kutoka mataifa maskini.
“Leo Rais Samia ni kiongozi anayeheshimika si Afrika pekee bali duniani kote. Hata kwenye mikutano ya wakubwa akisimama na kuzungumza, wote humsikiliza na vyombo vya habari huripoti kwa kina. Kuna mikutano ambayo ilihamia Afrika kwa mara ya kwanza kwa sababu ya Samia, kama ile ya nishati na mingine ya kimataifa. Dunia inaiangalia Tanzania kupitia yeye,” alisisitiza Sumaye.



