DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa Kimbunga “HIDAYA” kilichopo karibu na maeneo ya Pwani ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMA ya muda mchache uliopita imeeleza kuwa hadi kufikia saa 9 usiku wa kuamkia leo, Kimbunga “HIDAYA” kilikuwa katika eneo la bahari takriban kilomita 125 kutoka Pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi), kilomita 93 kutoka Pwani ya Mafia na kilomita 128 kutoka Pwani ya Dar es salaam kikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 985 na kasi ya upepo unaofika kilomita 120 kwa saa.
Tarrifa hiyo imeongeza kuwa tangu usiku wa kuamkia leo, matukio ya upepo mkali na mvua kubwa zinazosababishwa na uwepo wa kimbunga hicho yameendelea kujitokeza ambapo hadi kufika saa 3 asubuhi, kituo cha hali ya hewa cha Kilwa Masoko (Lindi) kimeripoti mvua ya jumla ya kiasi cha milimita 111.3 kwa kipindi cha masaa 6 yaliyopita.
Kiwango hiki cha mvua ni kikubwa sana ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko ni milimita 96.6 tu.
Hivyo kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya masaa 24 katika kituo cha Kilwa Masoko ni takribani asilimia 115 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko. Viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vingine katika kipindi hicho ni milimita 90.7 kwa Mtwara na milimita 85.3 katika kituo cha hali ya hewa Naliendele (Mtwara).
Kimbunga “HIDAYA” kinatarajiwa kuendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya nchi huku kikipungua nguvu taratibu kuelekea usiku wa kuamkia Jumapili Mei 05, 2024.