Taasisi yaandaa mkutano uwasilishaji bidhaa za kilimo

DAR ES SALAAM: TAASISI ya Vanguard Global Development imeandaa mkutano muhimu wa wadau utakaoangazia uwasilishaji wa Mpango wa Kitaifa wa Miundombinu ya Uhifadhi na Usafirishaji wa Bidhaa, hususan zile za kilimo, kwa lengo la kuongeza ushindani katika soko la taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,Mei27, 2025 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya taasisi hiyo, Mujwahuzi Alexander amesema kuwa mkutano huo utafanyika Juni 2, 2025, na utawakutanisha viongozi waandamizi wa serikali wakiwemo mawaziri kutoka wizara za Kilimo; Biashara na Maendeleo ya Viwanda; Mifugo na Uvuvi; pamoja na uchukuzi.
“Mbali na viongozi wa serikali, pia watakuwepo wadau kutoka sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, makampuni ya usafirishaji, wauzaji wa bidhaa nje ya nchi, pamoja na taasisi za maendeleo za kimataifa,” amesema Alexander.
Ameeleza kuwa mpango huo wa Kitaifa unalenga kuleta mapinduzi katika mnyororo wa thamani wa bidhaa zinazoharibika kwa haraka kama matunda, mboga mboga, samaki na nyama.
Kupitia miundombinu ya kisasa, bidhaa hizo zitaweza kuhifadhiwa na kusafirishwa kwa viwango vya juu na kwa ubora unaokubalika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Mpango huu unalenga kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa, kutoa msaada kwa wakulima, wavuvi na wazalishaji wa nyama zaidi ya 100,000, kuongeza uwezo wa nchi kutoa vyeti vya ubora na usalama wa bidhaa, pamoja na kujenga mfumo wa kisasa wa usafirishaji wa bidhaa zinazoharibika kwa kutumia teknolojia ya uhifadhi wa baridi kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi,” amefafanua Alexander.
Mkutano huo unatarajiwa kutoa dira ya utekelezaji wa mpango huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi wa kilimo na kuongeza ajira kupitia mnyororo wa thamani unaojikita katika usimamizi wa ubora, uhifadhi, na usafirishaji wa bidhaa.



