Taasisi yadhamiria mageuzi kilimo

DODOMA: TAASISI ya Heifer International Tanzania imeonesha dhamira ya kuleta mageuzi sekta ya kilimo kupitia ubunifu, ushirikishwaji na uwezeshaji wa vijana.
Akizungumza katika siku ya kwanza ya Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mshauri wa Ubora wa Maziwa kutoka Heifer International Tanzania, Ndisha Joseph amesema taasisi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kubadili maisha ya wakulima kupitia kilimo jumuishi na endelevu.

“Heifer inaamini kuwa kilimo bora ni kile kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, kinachowawezesha vijana, na kutoa suluhisho kwa changamoto za wakulima wa sasa. Ndiyo maana tupo Nanenane kuonesha teknolojia na mbinu bora zitakazosaidia jamii kufikia mafanikio,” amesema Ndisha.

Aidha, aliwaalika Wananchi kutembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo viwanja vya Nzuguni Dodoma, na pia Dole Kizimbani Zanzibar, kujionea ubunifu wa Heifer katika mifugo, kilimo biashara, na matumizi ya teknolojia kusaidia wakulima.




