Taasisi yatoa mbinu kilimo ikolojia

TANGA: ASASI isiyo ya kiserikali ya kijamii ENVIROCARE Tanzania,inayojihusisha na kukuza haki za mazingira, haki za binadamu, usawa wa kijinsia na mbinu endelevu za kilimo kwa wakulima, imetoa mafunzo kwa washiriki 44 mbinu bora za kutekeleza ili kupata suluhisho la kuboresha kilimo ikilojia.
Mafunzo hayo ya siku mbili yalifanyika katika kijiji cha Magoroto, wilaya ya Muheza, mkoa wa Tanga, ikiwa ni kilele cha Wiki ya Harakati za Kijani (GAW) iliyoandaliwa na ENVIROCARE.
Mratibu kutoka ENVIROCARE,Euphrasia Shayo amesema kuwa mafunzo hayo yalitolewa katika mashamba darasa ambayo yaliandaliwa kuonesha mbinu za vitendo za kilimo ikilojia.
“Mafunzo haya yaliwakutanisha washiriki 44 wanaume 23 na wanawake 21, wakiwemo vijana kwa lengo la kushirikishana maarifa na mbinu mbalimbali kupitia mashamba darasa ilikuwawezesha wakulima kupata uzoefu wa moja kwa moja katika kubaini changamoto za kilimo na kubuni suluhisho la kuzitatua,”amesema
Amesema mradi huo unatekelezwa katika kilele cha kampeni ya Green Action Week (GAW), iliyofadhiliwa na Swedish Society for Nature Conservation (SSNC).
Amesema kampeni hiyo ilihusisha shughuli mbalimbali ikiwemo mafunzo ya kilimo ikilojia, kilimo mchanganyiko, udhibiti wa wadudu wa asili katika mazao, uhifadhi wa maji mashambani, na uhifadhi wa bayoanuai katika mifumo ya ikolojia.
Euphrasia amesema mradi huo pia ulihusisha maofisa ugani wa kilimo kwa lengo la kushirikisha wakulima maarifa na ujuzi wa kitaalamu kuhusu mbinu za kuboresha usalama wa chakula, ikiwemo matumizi salama ya viuatilifu shambani na ufanyaji wa kilimo mchanganyiko.
“Maofisa ugani walitoa elimu kwa wakulima juu ya mbinu sahihi za kutambua ubora wa udongo na aina zinazofaa kwa kilimo, hususani wakati wa vipindi vya ukame. Pia walitoa elimu juu ya njia za kudhibiti upotevu wa maji mashambani ili kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuboresha usimamizi sahihi wa mazao,”amesema.
Euphrasia anaeleza kuwa mradi huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mshikamano kati ya wakulima, maafisa ugani, wanawake na vijana, sambamba na kupanua uelewa wao kuhusu kilimo endelevu na usalama wa chakula. Wakati huo huo, umesaidia kuimarisha jitihada za kukuza kilimo endelevu na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Anaongeza kuwa, licha ya kuwepo kwa Mkakati wa Taifa wa Kilimo Hai cha Ikilojia (NEOAS), utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua kutokana na upungufu wa bajeti, uelewa mdogo wa wakulima na maafisa ugani, pamoja na changamoto za kifedha katika kupata ujuzi wa muda mrefu juu ya kilimo endelevu.
“Hali hii imewalazimisha wakulima wadogo wengi kuendelea kutumia mbinu zisizo endelevu, ambazo zinahatarisha usalama wa chakula katika ngazi ya kaya na mazingira kwa ujumla,” anafafanua Euphrasia.
“Kwa kuwapa washiriki ujuzi wa vitendo na kuwapatia jukwaa la fursa za kujifunza, jitihada hizi zimeziwezesha jamii kuelewa kwa undani umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na usimamizi sahihi wa usalama wa chakula. Kusisitiza mbinu za kilimo ikilojia basi ni msingi wa kila mmoja, kwa lengo la kuboresha mifumo ya lishe na kuinua maisha ya wote,” anaongeza.
Kwa upande wake Ofisa Ugani wa Kilimo, Seif Rashidi anasema kampeni hiyo imeisaidia kukuza masuala ya jinsia na ushirikishwaji wa vijana katika kilimo kwa kuhamasisha kushiriki kwenye vipindi vya redio na kuchapisha makala katika vyombo vya habari ili kueneza ujumbe kwa wananchi wa Magoroto.