Taasisi zaongezwa miezi 5 kupika kwa nishati safi

SERIKALI imeagiza taasisi zikiwemo shule zenye wanafunzi zaidi ya 100 ziache kutumia kuni na mkaa ifikapo Juni mwaka huu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa agizo hilo wilayani Maswa katika Mkoa wa Simiyu jana.
Majaliwa alisema awali baadhi ya taasisi zilitakiwa kufikia ukomo wa matumizi ya kuni na mkaa Desemba, mwaka jana lakini zimeongezewa muda hadi Juni mwaka huu ili kuingiza mpango huo katika bajeti ya kuanzia Januari hadi Juni.
“Taasisi zinazokutanisha wanafunzi wengi, wasomi wengi, watu wengi kuanzia mia na kuendelea hawa ni lazima wabadili Teknolojia yao ya kupikia chakula chao watumie umeme, gesi au makaa yanayotokana na vumbi yanayotengenezwa na wataalamu lakini sio makaa ya miti,” alisema.
Aliongeza: “Muda wao ulishakwisha Desemba tumewapa tena miezi mitano ili sasa waingize kwenye bajeti ile ambayo sasa itakwenda hadi Juni ambayo juzi imeridhiwa kufanyiwa mabadiliko ya bajeti, ikifikapo Juni taasisi zote zinazokaa na wanafunzi zaidi ya mia ziwe zinatumia gesi au umeme”.
Majaliwa alisema matumizi ya nishati safi katika kupikia yatasaidia kupunguza kukatwa kwa miti inayotumika kwa ajili ya kuni au mkaa.
Michango shuleni
Alisema serikali imeendelea na msimamo wake wa kuondoa michango mashuleni ambayo imekuwa kero na kikwazo kwa baadhi ya watoto kupata elimu na kuwataka wazazi na walezi kwenda kuwaandikisha watoto shule ili wapate elimu.
“Ipo michango rasmi ambayo inasimamiwa na wakuu wa wilaya tu na si mtu mwingine hata kama mtapanga huko kujenga choo lazima mumjulishe mkuu wa wilaya ili mnaposema tunataka kuchangisha atafakari mchango huo kama ni mchango unakwenda kutumika vizuri,” alisema.
Vilevile, Majaliwa alihimiza wenye sifa ya kupiga kura wajitokeze kuhakiki taarifa zao katika daftari la wapiga kura ili wapate fursa ya kuchagua viongozi watakaowaongoza katika kupindi cha miaka mitano ijayo.
Aliwataka pia wananchi washirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama kudumisha amani na utulivu kwa kuwafichua wahalifu katika maeneo yao pamoja na watu wanaofikia katika nyumba za wageni kuadika majina yao kwa sababu za kiusalama.
“Kama analala nyumba ya wageni ni nani huyo aandike tumjue aweke kumbukumbu kama ni mtu mwema atafanya hivyo kama si mwema ataacha kuandika, mbona mimi nikija Maswa naandika kwenye daftari maalumu la wageni, kwamba mimi Kassim Majaliwa nimekuja hapa leo,” alisema Majaliwa.
Aidha, alihimiza wananchi hasa wanaume wapime afya zao ili kujua kama kuna changamoto waweze kuanza tiba na waache tabia ya kuwategea wenza wao kupima.
“Najua sisi wanaume huwa hatupimi tunategemea majibu ya wake zetu, yaani mkeo akienda kupima akiambiwa hana na wewe unafurahi na siku hiyo unakwenda kunywa bia hapana wewe kapime kivyako,” alisema Majaliwa.