TADB yachochea kilimo cha kisasa Kibaha

KIBAHA, Pwani: Kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetembelea kikundi cha wakulima cha Wazito Farm Flex kilichopo Kibaha, Mkoa wa Pwani, na kukabidhi msaada wa pembejeo pamoja na zana mbalimbali za kilimo.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Ofisa Mwandamizi wa Huduma kwa Wateja kutoka TADB, Faithful Joshua, alisema kaulimbiu ya wiki ya huduma kwa wateja mwaka huu ni “Mission Possible” ikimaanisha kufanya lisilowezekana kuwazekana.

“Ndiyo maana tumeamua kuwasaidia wakulima hawa ili waweze kuendeleza kilimo bora na cha kisasa kitakachowawezesha kukuza uchumi wao na kuchangia maendeleo ya taifa,” alisema Joshua.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa kikundi hicho, Habraman Othman, aliishukuru TADB kwa kuwatembelea na kuwapatia vitendea kazi.

“Tunashukuru sana TADB kwa msaada huu. Tunaahidi kuongeza juhudi katika kilimo ili kuongeza uzalishaji na kupata mazao mengi zaidi,” alisema Othman.

TADB imeendelea kujipambanua kama benki shirikishi inayowawezesha wakulima wadogo na wa kati nchini, kupitia huduma za kifedha na misaada ya vitendea kazi ili kuchochea mapinduzi ya kilimo Tanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button