TADB yaipa serikali gawio bil 6/-

DAR ES SALAAM – BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa gawio la Sh bilioni 5.58 kwa serikali katika mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31, mwaka jana.

Gawio hilo ni zaidi ya mara tano ya Sh milioni 850 kwa mwaka ulioishia Desemba 31, 2023 ikiwa limeongezeka kwa asilimia 556.

Akizungumza baada ya mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege alisema benki yake imefanya vizuri baada ya serikali kuiongezea mtaji wa Sh bilioni 174 mwaka jana.

“Kwa sababu mtaji ulikuwa umeongezeka ikatufanya tukafanya vizuri zaidi, ikakuza mali za benki kutoka Sh bilioni 607 kwa mwaka 2023 mpaka Sh bilioni 917 mwaka 2024 ni ongezeko la asilimia 61,” alisema.

Mapato hayo ikilinganishwa na taasisi nyingine za kifedha hakuna taasisi yenye ukuaji wa asilimia 61 kwa mwaka mmoja. Alisema mbali na mali, pia mikopo iliongezeka kutoka Sh bilioni 331 kwa mwaka 2023 mpaka Sh bilioni 534 kwa mwaka 2024.

“Hilo pia bado ni ongezeko kubwa la zaidi ya asilimia 51, hii yote ni sababu ya uwezeshwaji uliofanywa na serikali kutuongezea mtaji,” alisema.

“Toka Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani imetuongezea mtaji kwa kiasi kikubwa sana, mara ya kwanza Rais (Samia Suluhu Hassan) alipoingia madarakani alituongezea mtaji wa Shilingi bilioni 208 na mwaka jana kama nilivyosema alituongezea mtaji wa Shilingi bilioni 174 na mtaji wetu ukakua kutoka Shilingi bilioni 60 mpaka Shilingi bilioni 442,” alisema.

Alisema hayo yote yanaifanya benki hiyo kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi zake na ndio maana kwenye kikao cha jana walionesha kuridhika na walichopatiwa na serikali kwa kutoa gawio hilo.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama aliipongeza benki hiyo na kusisitiza kuwa taasisi hiyo ni ya kisera yenye mkakati wa kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo ikiwemo mifugo na uvuvi kupitia mikopo na mitaji yenye masharti nafuu.

“Katika vigezo vya kiuwekezaji, fedha benki imeonekana kufanya vizuri kwani ukuaji wake wa mali za benki umekuwa kwa kiasi kikubwa sana, hii ni dalili nzuri kwamba benki inaendelea vizuri na hii inaondoa dhana kwamba benki za serikali si nzuri,” alisema.

Alisema serikali inafurahia uwekezaji katika benki hiyo kwani ni moja ya mafanikio yake makubwa na mpango wake (serikali) ni kuona inaendelea kuwekeza kwani imeleta tija.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button