TAFEYOCO: Tutumie uchaguzi kuimarisha umoja na amani

DAR ES SALAAM: SHIRIKA la Vijana na Wanawake Tanzania (TAFEYECO) limewataka wananchi kutumia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 kama fursa ya kuimarisha umoja, amani na maendeleo ya taifa, badala ya kugawanyika kutokana na taarifa potofu zinazochochewa mitandaoni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TAFEYOCO, Elvis John, amesema utafiti uliofanywa na shirika hilo katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kupitia mfumo wa Open Data Kit (ODK) umeonesha kuwa asilimia 64 ya wanawake na 36 ya wanaume walishiriki kutoa maoni kuhusu wagombea wa urais na matarajio yao kwa serikali ijayo.
Amesema, wengi wa walioshiriki wamependekeza serikali ijayo iwe na Baraza la Mawaziri lenye uwiano, likijumuisha viongozi wa vyama vya upinzani, pamoja na kuanzishwa kwa kamati ya maridhiano ya kitaifa itakayowashirikisha Watanzania waliopo ndani na nje ya nchi.
“Wananchi wameonyesha kiu ya kuona Tanzania inasonga mbele kwa umoja na maridhiano. Wamependekeza pia kuwepo kwa sheria kali zitakazodhibiti matumizi mabaya ya mitandao na upotoshaji wa taarifa,” amesema Elvis.
Aidha, amebainisha kuwa maoni mengine yamegusia mahitaji ya ujenzi wa barabara za juu katika maeneo yenye msongamano ili kurahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Kwa upande wao, wanachama wa TAFEYOCO, Jesca John na Magreth Ndomba wamewahimiza vijana kote nchini kujitokeza kupiga kura kwa wingi siku ya uchaguzi, wakisema ni njia halali ya kuchagua kiongozi atakayesimamia maslahi ya taifa.
“Vijana tusiruhusu kutumika vibaya kwenye maandamano au propaganda zisizo na tija. Tunahitaji viongozi watakaotuletea maendeleo, si migawanyiko,” amesema Magreth.
Naye mmoja wa washiriki wa utafiti huo amesema, “Hatuna nchi nyingine. Tunapaswa kuwa makini na taarifa tunazopokea na kutumia uchaguzi huu kama chombo cha kujenga Tanzania tunayoitaka.”
TAFEYOCO imesisitiza kuwa matokeo ya utafiti huo ni ishara kuwa wananchi wanatamani kuona uchaguzi wa amani, maridhiano na maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.