TALIRI yaja na ufumbuzi malisho kwa wafugaji

DAR ES SALAAM; TAASISI ya Utafiti wa Mifugo Tanzania ( TALIRI), imesema ili kufuga kisasa, inahitajika malisho ya kutosheleza kwa mwaka mzima.

Mtafiti Mwandamizi kutoka Taliri, Walter Mangesho amesema hayo kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Dar es Salaam.

Mangesho amesema taasisi hiyo imezalisha mbegu za malisho bora ya nyasi aina ya ‘Cencrus Ciliaris’, ambazo zimefanyiwa utafiti na kuonekana kufanya vizuri kwenye maeneo mengi nchini kwa kuwa yana uwezo wa kustahimili ukame.

Advertisement

Amesema kwa kuwa yanastahimili ukame yanaongeza uzalishaji wa maziwa kutokana na viini lishe vilivyopo kwenye nyasi hizo.

Amesema malisho haya yana uwezo wa kuzalisha na kutoa takribani tani sita hadi 10 kwa ekari moja kwa mwaka, yanaoteshwa kwa kutumia njia ya vipando au kwa njia ya mbegu.

Soma pia:https://habarileo.co.tz/pinda-ataka-teknolojia-zitakazosaidia-wafugaji/

“Yanaweza kuhifadhiwa hali ya ukavu yakiwa kwenye robota yakiwa na uzito wa takribani kilo 18, ambazo kwa wastani zinaweza kutumiwa na ng’ombe mmoja au wawili kwa siku huku ng’ombe wa maziwa mwenye uzito wa kilo 250 hadi 300 anaweza kula robota moja kwa siku mbili.

“Aina nyingine za nyasi zinaitwa Napier, mabingobingo na juncao nazo zinafanya vizuri kwenye maeneo yenye milima au sehemu zenye maji maji huku yakiwa na uwezo wa kuzalisha tani 8 hadi 16 kwa ekari moja kwa mwaka,” amesema.

Amewataka wadau wa mifugo kutembelea banda hilo, ili kujifunza kwa undani namna ya lishe, ulishaji wa mifugo pamoja na teknolojia mbalimbali za mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo kwa lengo la kuongeza tija kwenye uzalishaji.