TAMISEMI: Kuna mageuzi makubwa sekta ya elimu
DODOMA — Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imetangaza mafanikio makubwa katika sekta ya elimu ya msingi na sekondari, ikiwemo uwekezaji mkubwa katika miundombinu, ajira kwa walimu, na ongezeko la ushiriki wa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Akihutubia Bunge jijini Dodoma, Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa alisema serikali imefanya mabadiliko ya kweli ambayo yanagusa maisha ya kila mtoto wa Kitanzania.
“Leo ninatoa ushahidi wa mabadiliko ya shule zilizofufuliwa, walimu walioajiriwa, watoto waliowezeshwa, na matumaini mapya yaliyochipuka kila pembe ya nchi yetu,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, serikali imeboresha shule 28 za mchepuo wa elimu ya ufundi kwa kuzikarabati na kuzipatia vifaa vya kisasa, sambamba na kuboresha shule 274 za kilimo na 28 za biashara.
Aidha, idadi ya miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu, mabweni na mabwalo imeongezeka kutoka vipengele 582,733 hadi 754,075.
View this post on Instagram
Katika kuhakikisha elimu inapatikana kwa wote bila kikwazo cha ada, ruzuku ya Elimu Bila Ada imeongezeka kutoka Sh bilioni 249.66 hadi Sh bilioni 484.27 kwa mwaka – sawa na ongezeko la asilimia 94.
Pia, watoto wenye mahitaji maalum wameongezeka kutoka 28,482 hadi 78,429 sawa na asilimia 175. Serikali imejenga madarasa 44, matundu ya vyoo 132 na mabweni 172 mahsusi kwa kundi hilo.
Waziri Mchengerwa aliongeza kuwa serikali imeajiri walimu 44,527, wakiwemo 447 wa elimu maalum, ili kuboresha utoaji wa elimu jumuishi.
“Matokeo haya si tu mafanikio ya kiutawala, bali ni ushindi wa kitaifa. Haya ni matendo yanayosema kwa sauti kubwa kuliko maneno: kwamba serikali hii haikuja kuahidi tu, bali kutekeleza,” alisisitiza.
PIA SOMA: Serikali: BRT sasa kuendeshwa kwa ubia na sekta binafsi
Kwa mujibu wa Waziri, dhamira ya serikali ni kuhakikisha kila darasa linalojengwa si tu ukuta, bali ni mlango wa maisha mapya kwa kila mtoto wa Kitanzania.
Mageuzi haya yanadhihirisha kwamba elimu ni kipaumbele cha taifa na chombo kikuu cha kuinua maisha ya wananchi wote.



