Tani 196,000 za korosho zasafirishwa bandari Mtwara

WAKATI msimu wa uuzaji wa korosho mwaka 2024/2025 ukiendelea, Bandari ya Mtwara imesafirisha tani 196,000 korosho ghafi, Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa anasema.
Mbarawa amesema hayo leo wakati wa ziara yake bandarini hapo na kuongeza kuwa hatua hiyo imetokana na uwekezaji ambao umeongeza ufanisi wa bandari.
“Mwaka mmoja uliopita, ulikuwa unakuta meli moja kila siku, lakini kwa sasa mnaona kama leo kuna meli mbili zinapakia korosho tu na kesho kutakuwa na meli nyingine tatu, haya ni mabadiliko makubwa,” amesema.
Mbarawa amesema mabadiliko hayo yamekuja kutokana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kuborasha ufanisi wa bandari nchini.
Amesema serikali imeongeza vitendea kazi vingi sana kwenye Bandari ya Mtwara vingi vikiwa vimehamishwa kutoka bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ufanisi wa bandari hiyo ya Mtwara.
Katika hatua nyingine Mbarawa amewataka wafanyakazi wa bandari kuongeza ufanisi katika kupanga magari, kuandaa na kusimamia upakuajia na upakiaji wa mizigo ili kupunguza siku za meli kukaa bandarini.



