Tanzania, Finland kuboresha ujasiriamali nchini

DAR ES SALAAM: UBALOZI wa Finland nchini umesema utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuongeza umuhimu wa matumizi ya mifumo ya kidijiti kwa vijana wajasiriamali ili kuboresha huduma za umma na ujasiriamali.
Balozi wa Finland nchini, Theresa Zitting alisema hayo jana Dar es Salaam kwenye warsha ya wiki ya Nordiki 2025 yenye lengo la kukuza ubunifu endelevu na matumizi ya kidijiti katika ujasiriamali kwa vijana.
Alisema Mwaka huu, wameangazia uendelevu, mabadiliko ya kidijiti na ubunifu kwa wanafunzi, wajasiriamali, washauri wa biashara na waendelezaji wa mazingira ya ubunifu ili kuona umuhimu wa mawasiliano katika kuongeza thamani ya ubunifu kwa vijana wajasiriamali.
Alieleza kuwa warsha hiyo imeandaliwa kwa vijana wajasiriamali kwa sababu ya kukua kwa kasi kwa matumizi ya kidijiti yanayobadilisha namna ya kuishi,kufanya kazi na kuwasiliana.
SOMA ZAIDI:
“Tuko hapa kwa sababu ubunifu hauwezi kustawi katika kimya yanahitajika mawazo bora ili kuona ambavyo kila kijana anavyoweza kuwasilisha wazo la biashara yake na jinsi ya kuliboresha ili kuvutia wateja na kupata ufadhili watakao mshika mkoto kufikia ndoto yake na kwa ajili ya kufikia soko la kimataifa,” alisema Balozi Zitting.
Alisema ubunifu wa kidijiti una nguvu ya kuifikia dunia kwa sasa na unatoa fursa mpya za ukuaji wa uchumi jumuishi, huduma bora kwa umma, na suluhisho bunifu kwa kutatua changamoto ya teknolojia ya fedha, afya, kilimo na kuchochea maendeleo endelevu na kuunda ajira kwa kizazi kipya kwa ajili ya ustawi wa jamii na taifa.
Pia alisema kwa kuwa bunifu si safari ya mtu mmoja Nchi za Nordiki ziko tayari kushirikiana na jamii ya wabunifu wa Tanzania kwa sababu wanatambua ushirikiano huo haupaswi kuishia kwenye ufadhili tu bali unapaswa kujengwa kwenye msingi wa ushirikiano wa watu, kampuni, na taasisi.
Alieleza kuwa Finland na nchi zingine za Nordiki, wamejifunza kuwa mazingira ya ubunifu yanaweza kustawi panapokuwepo fursa za kujaribu kutoa mawazo kwa watu wengine, kujenga biashara, na kutatua matatizo yaliyopo kwa kushirikisha watu.
Balozi Zitting alisema kupitia programu mbalimbali, ikiwemo Tanzania ICT Programu iliyoanzishwa 2010, Finland imekuwa ikishirikiana kwa karibu na wadau wa Tanzania kuimarisha mfumo wa kidijitali, kukuza ubunifu jumuishi, na kuwaunga mkono wajasiriamali kwa vitendea kazi na mwonekano wa bidhaa zao.
“Wakati wa kushirikiana huwa tunachunguza fursa kwa pamoja, mara nyingi kwa msaada kutoka Finnpartnership—mpango unaosaidia kufanikisha ushirikiano wa biashara na kutoa msaada wa kifedha kwa miradi ya pamoja. Ushirikiano huu ni muhimu kwa kuunda ajira, kushirikisha maarifa, na kubuni suluhisho zinazoweza kufanyika kwa kiwango kikubwa,” alisema.
Aidha alisema anaamini nguvu kubwa ya Tanzania ipo kwa watu wake hasa vijana walioelimika na wenye ndoto kubwa hivyo alitoa wito wa sekta za kidijitali zinatoa njia za ajira na ushiriki wa kimataifa kuunganisha vyuo vikuu na ujasiriamali ili kuwaanda vijana mapema na ujasiriamali.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wajasiriamali wa Tanzania, Zahoro Muhaji alisema warsha hiyo imewasaidia vijana kuelezea mawazo ya biashara zao na kupata ufadhili wa kuendeleza miradi yao.
Naye mmoja wa vijana waliowasilisha wazo bunifu, Rebeka Kitenge alisema warsha hiyo imemuwezesha atambue namna ya kuwaslisha wazo kwa wawekezaji ili kupata msaada kutoka kwa wafadhiri.
Alisema baada ya kupata maoni kutoka kwa jopo la majaji sasa anaenda kuboresha kile alichoshauliwa katika ubunifu wake wa kutengeneza sabuni za maji za kufulia ili aweze kuwa na bidhaa itakayoleta ushindani kimataifa.
Warsha hiyo ilihusisha wajasiriamali wa Tanzania, watunga sera, mashirika ya ubunifu ya nchi za Nordic ambazo ni Finland, Sweden,Dermark na Norway, viongozi wa mazingira ya ubunifu ikilenga kuchunguza jinsi ya kutumia mawasiliano madhubuti katika kukuza biashara ndogo, kuongeza mwonekano, na kuanzisha ushirikiano wa kimataifa.



