Tanzania imeng’ara Afrika

MKUTANO wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati ulihitimishwa jana Dar es Salaam.
Tunapongeza hatua hii ya Tanzania kuandika historia Afrika kuwa mwenyeji wa mkutano huu mkubwa.
Tanzania imeng’ara si tu kwa kuratibu kwa mafanikio mkutano huu, bali pia kwa kujizolea sifa kwa ukinara wa matumizi ya nishati safi Afrika.
Tunapongeza kwa dhati mkutano huu kufanyika kwa siku mbili kisha kuhitimishwa salama hatua ambayo imezidi kuipaisha Tanzania chini ya uongozi madhubuti wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kitendo cha nchi na Rais Samia kusifiwa kwa uwazi mbele ya maelfu ya wajumbe wa mkutano huo, hakika kimewajengea ujasiri Watanzania kiasi cha kutembea kifua mbele wakiamini ambavyo nchi inasonga mbele na kuaminika kimataifa.
Mkutano huu umezidi kuionesha nchi inavyong’ara hata kidiplomasia kiasi cha kuipa jukumu kubwa kuwa mwenyeji na ukafanyika kwa amani, utulivu na mafanikio makubwa.
Ni fahari kwa Watanzania kuona taasisi za kimataifa ikiwamo Umoja wa Mataifa (UN), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kupitia mkutano huo, zikitambua mafanikio ya Tanzania katika kufikisha umeme vijijini.
Naibu Katibu Mkuu wa UN na Mwenyekiti wa Timu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed alinukuliwa katika mkutano huo akisema, “Tanzania imekuwa ni nyota inayong’ara katika kuhakikisha kunakuwepo na umeme wa kutosha vijijini pamoja na kuleta mabadiliko na mapinduzi makubwa ya umeme hasa kwa maeneo ya vijijini”.
Mkutano huu umetoa jukwaa zuri kuweka wazi mafanikio ya Tanzania mbele ya dunia na hata kuwa mfano wa kuigwa katika Afrika.
Hata hivyo, haya si matokeo ya bahati, ni utendaji na uthubutu wa serikali chini ya uongozi thabiti wa Rais Samia.
Serikali imedhihirisha kwa vitendo kutumia rasilimali zake kwa ubunifu kuleta maendeleo kupitia nishati safi.
Zaidi ya hayo, mkutano huu umetoa fursa kwa viongozi na wakuu wa nchi zilizoshiriki kujifunza kwa mafanikio ya Tanzania, na kujadili mikakati ambayo inaweza kusaidia kueneza matumizi ya nishati safi katika mataifa yao.
Kwa hivyo, si tu kwamba Tanzania imejijengea hadhi ya kimataifa, bali pia imefungua milango kwa ushirikiano wa kikanda utakaoleta manufaa kwa wote.
Jana akihitimisha mkutano huo, Rais Samia alisema kupitia mpango mahususi wa kitaifa wa umeme kwa nchi za Afrika, Tanzania itahitaji Sh trilioni 33 na kuongeza kasi kuunganisha umeme nchini hadi kufikia asilimia 72 ifikapo mwaka 2030.
Tunaamini ni wakati muafaka kwa nchi za Afrika kuiga mfano wa Tanzania, kuhakikisha umeme unapatikana kwa
wote, na matumizi ya nishati safi yanapanuka.
Tunaendelea kuipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu, kuuhitimisha salama na kuendelea kuwa kinara wa matumizi ya nishati safi.
Hatua hii ni uthibitisho tosha wa uwezo wa Tanzania kujenga jamii endelevu kwa kutumia rasilimali zake kwa maendeleo endelevu.



