Tanzania, Japan kukuza biashara, uwekezaji

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na  wale wa mataifa mengine, ikiwemo Japan ili kunufaika na fursa za kimataifa kupitia ushiriki wa nchi kwenye makongamano ya biashara, uwekezaji na utalii.

Majaliwa ameyasema hayo alipofungua Kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii lililowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Japan jijini Osaka, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania kwenye maonesho ya World Expo Osaka 2025.

Alisema Tanzania imekuwa ikinufaika na mikutano kama hiyo, ambayo imeongeza ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Alisema hadi Machi 2025, kampuni 24 kutoka Japan zimewekeza Tanzania kwenye miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 42.7 na kuwapatia ajira Watanzania 1,182.

Pia, alisema serikali imenufaika na misaada kutoka Japan katika miradi ya maendeleo hususani kilimo na miundombinu.

Katika kongamano hilo, hati sita za ushirikiano zilisainiwa, zikiwemo kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la JGC la Japan kuhusu sekta ya mafuta, TIC na Axcel Afrika, ZIPA na Axcel Afrika, TGDC na Toshiba, Shirika la Tiba la Tokushukai na Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Hospitali ya Benjamin Mkapa na AFRECO kwa kushirikiana na taasisi hizo mbili.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo alisema dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uwekezaji inaendelea kuzaa matunda na kwamba sekta za biashara, miundombinu, utalii, uchumi wa buluu, kilimo na madini zimepewa kipaumbele kwa ushirikiano na Japan.

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanza kujenga miundombinu ya mitaa ya viwanda Duga Zuze na Chamanangwe, Pemba na kuzindua jarida la fursa za uwekezaji lililogawiwa kwa wawekezaji wa Japan.

Kamishna Jenerali wa World Expo Osaka 2025 kwa Tanzania na Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis nalisema kongamano hilo linaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na Japan kwenye sekta za nishati, madini, kilimo, huduma za kifedha, afya, utalii na uwekezaji ili kukuza ushirikiano wa kibiashara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button