Tanzania, Kenya zaondoa vikwazo 4 vya biashara

TANZANIA na Kenya zimeondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kiushuru vinne kati ya 14 vilivyojadiliwa katika Mkutano wa Tisa wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya nchi hizo.
Hatua hiyo inatimiza vikwazo 58 vilivyotatuliwa kati ya 68 vilivyokuwepo, huku vikwazo 10 vilivyobakia vitatatuliwa Machi 31, 2026.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah amesema hayo wakati wa mkutano huo uliofanyika Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, nchi hizo mbili zimejadili vikwazo hivyo na kutia saini makubaliano ya kutimiza makubaliano yaliyowekwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya, Dk William Ruto, wakati wa ziara nchini Tanzania Oktoba 9–10, 2022 kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa biashara baina ya nchi hizo.
Aidha, Dk Abdallah amebainisha vikwazo vilivyoondolewa vikijumuisha kuondoa kodi ya zuio kwa bia za Kampuni ya Bia Tanzania(TBL) kwenda Kenya na mihuri ya ushuru.
Pia, ada na utaratibu wa usafirishaji wa bidhaa za mifugo kutoka Kenya kutekelezwa kwa kufuata maamuzi ya Baraza la Kisekta la Fedha na Uchumi la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kuondoa bima ya COMESA kwa kuwa haihusiani na Tanzania.
Amesema nchi hizo zimeahidi kushirikiana katika kuhakikisha biashara kati ya Tanzania na Kenya inafanyika kwa haki, kwa kuzingatia mikataba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kuwasilisha masuala mapya kupitia njia za kidiplomasia ndani ya mwezi mmoja baada ya mkutano huo.
“Tumekubaliana ndani ya miezi sita, ifikapo Machi 31, 2026 vikwazo vyote vitakuwa vimekwisha na suluhu zao zitatolewa kikamilifu. Kila sekta na idara ina jukumu la kukutana na upande wa pili, kujadiliana kwa pamoja na kutafuta njia za kudumu za kuyatatua. “Wataalamu pia wanashirikiana kwa karibu kusaidia wafanyabiashara kuhakikisha biashara inafanyika kwa urahisi na ufanisi,” amesema.
Katibu Mkuu wa Biashara katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya, Regina Ambam ameeleza kuwa makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kurahisisha mifumo na kuweka mazingira bora kwa wafanyabiashara wa Afrika Mashariki na ustawi wa wananchi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kujiandaa kwa biashara ya kidijiti na ni hatua ya kihistoria katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kuchochea ujumuishaji wa kikanda na kuiweka Afrika Mashariki katika nafasi ya ushindani duniani.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Kenya, Carolyne Karugu amesema kamati hiyo ya pamoja imefanikiwa kuondoa vikwazo hivyo vya biashara visivyo vya kiushuru kwa asilimia 78, yanatokana na makubaliano yaliyowekwa wakati wa ziara rasmi ya marais wa nchi hizo mbili.



