Tanzania kuimarisha diplomasia AU

RAIS Samia Suluhu Hassan yuko jijini Addis Ababa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia kushiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU). Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu iliyotolewa jana Dar es Salaam ilieleza kuwa mkutano huo wa Addis Ababa utafanyika kwa siku mbili kuanzia Februari 14, mwaka huu.
Machumu ameeleza kuwa katika mkutano huo, Tanzania inalenga kuendelea kuimarisha nafasi yake katika diplomasia ya kikanda na kimataifa, kutetea maslahi ya taifa na kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Afrika yenye amani, mshikamano, uthabiti wa kiuchumi na maendeleo endelevu.
Ameeleza kuwa katika mkutano huo, Rais Samia amependekezwa kuteuliwa kuwa kinara wa AU katika masuala ya afya ya mama na mtoto, na uteuzi huo unatarajiwa kupitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali. “Uteuzi huo unaakisi dhamira ya Tanzania katika kuimarisha huduma za afya, ustawi wa familia na maendeleo ya rasilimaliwatu barani Afrika,” alieleza Machumu.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU ni chombo cha juu zaidi cha uamuzi cha AU chenye mamlaka ya kupitisha maazimio, matamko na mwelekeo wa sera za Afrika. Machumu ameeleza Tanzania inakamilisha muda wake wa kuhudumu katika Baraza la Amani na Usalama la AU baada ya kulitumikia kwa vipindi viwili mfululizo kuanzia mwaka 2022 hadi 2026, hivyo kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha amani, utulivu na usalama Afrika.
Mkutano huo utatangaza uongozi wa AU kwa mwaka 2026 na utamthibitisha Mwenyekiti mpya endapo Rais wa Jamhuri ya Burundi, Évariste Ndayishimiye atachaguliwa.Mwenyekiti mpya ataongoza AU mwaka 2026, akipokea kutoka kwa mwenyekiti wa mwaka 2025 anayemaliza muda wake, Rais wa Jamhuri ya Angola, João Lourenço.
Nafasi ya mwenyekiti wa AU hupatikana kwa utaratibu wa mzunguko wa kanda ili kila eneo la Afrika lipate fursa ya kuongoza umoja huo. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Mwenyekiti, ikiwakilisha Kanda ya Mashariki.
Machumu ameeleza kwamba nafasi hiyo inaakisi imani ya nchi wanachama kwa mchango na uongozi wa Tanzania katika masuala ya Bara la Afrika. Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika utaongozwa na Kaulimbiu: “Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji na Huduma Salama za Usafi wa Mazingira ili Kufikia Malengo ya Ajenda 2063.” “Kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza hatua za pamoja za bara katika kuhakikisha usalama wa rasilimali maji, afya ya jamii na maendeleo endelevu,” alieleza Machumu.

Rais Samia anatarajiwa kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC) utakaofanyika chini ya uenyeji wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto. Baadaye leo Rais Samia atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Abiy Ahmed Ali.
Pia, anatarajiwa kuzungumza na viongozi kadhaa: Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini, Russell Dlamini; Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Azali Assoumani; Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Amina Mohammed na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.SOMA: Samia ahimiza kuomba amani, ustahimilivu



