Tanzania mfano bora uhuru soko la pamoja EAC

TANZANIA imeendelea kutekeleza kwa vitendo Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa maslahi ya watu wa Afrika Mashariki na ukuaji wa uchumi wa kanda hiyo.
Tukio la hivi karibuni la kuzuiwa bidhaa za kilimo kutoka Tanzania na mataifa ya Malawi na Afrika Kusini ambayo sio wanachama wa EAC, ni kielelezo cha utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja kutokana na hatua ilizochukua.
Ikumbukwe kuwa baada ya kuwekewa vikwazo vya bidhaa zake za kilimo na mataifa hayo, Tanzania iliweka wazi kuwa sio nia yake kuingia katika vita vya kibiashara hivyo kutoa siku sita kwa mataifa hayo kuondoa zuio hilo kidiplomasia.
Kitendo cha kukataa kuchukua hatua ya moja kwa moja ya kulipiza kisasi kwa kufunga milango kwa nchi hizo na badala yake kutoa muda kwa nchi hizo kujitafakari, kimeifanya Tanzania kuwa mshirika bora anayeheshimu na kutekeleza itifaki kimataifa.
Ni kweli kuwa hata vikwazo vilivyotangazwa na Tanzania vilisababishwa na nchi hizo kukaidi ombi la Tanzania la kuondoa zuio hilo kwa bidhaa za kilimo kutoka Tanzania.
Aidha, baada ya nchi hizo kutangaza kuondoa zuio hilo Tanzania haikuwa na chaguo lingine zaidi ya kuondoa marufuku iliyoiweka kwa bidhaa za kilimo kiutoka katika nchi hizo.
Tunaipongeza Wizara ya Kilimo chini ya Waziri Hussein Bashe kwa kuendelea kutekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja ndani ya EAC na Afrika kwa ujumla.
Wizara ya Kilimo imesimamia vyema suala hilo na kutunza weledi wa Tanzania na kuifanya nchi kushinda katika majaribu hayo.
Ni matarajio yetu kuwa Tanzania itaendelea kutekeleza Itifaki zote za EAC hali itakayochochea maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, viwanda na miundombinu.
Kadhalika, soko la pamoja litaimarisha uwezo wa nchi za EAC kukabiliana na mbinu mbalimbali za kiuchumi za mataifa makubwa duniani kwa kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Tunaamini vikwazo vya kiuchumi hasa katika mazao ya kilimo katika nchi za EAC katika miaka ya nyuma havitajirudia bali tunachohitaji kwa sasa ni kusonga mbele kibiashara na uwekezaji kwa kuimarisha sera, sheria na kanuni katika kuyafikia masoko yetu.
Ni dhahiri kuwa kuweka masoko wazi kwa kufuata taratibu za kiforodha ni njia moja wapo inayowajenga wajasiriamali wa Tanzania na EAC kwa ujumla kiuchumi kutokana na uuzaji wa bidhaa mbalimbali katika kanda.
Tunaipongeza serikali ya Tanzania kwa kusimamia taratibu za kiforodha na kuona siku zote soko linaheshimiwa na kuwa wazi kwa wafanyabiashara wa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Ni vizuri viongozi wa nchi zote za EAC kuiga mfano wa Tanzania katika kusimamia soko la pamoja kwa kuweka milango ya soko lake wazi kwa wafanyabiashara wa EAC na kanda zingine kwa sababu kwa kufanya hivyo inakuza uchumi wa watu wake na kanda kwa ujumla.