Tanzania mwenyeji Mkutano Mkuu Viwango Afrika

DAR ES SALAAM: TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu wa Shirika la Viwango Barani Afrika (ARSO) utakaofanyika Zanzibar kuanzia Juni 23 hadi Juni 27, 2025.
Mkutano huo unaotaratibiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), unalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kutangaza bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 27, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Ashura Katunzi, amesema kuwa mkutano huo utawakutanisha wageni takribani 300 kutoka zaidi ya nchi 50, wakiwemo wanachama wa ARSO na wadau mbalimbali wa viwango kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika, huku mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Katunzi amebainisha kuwa fursa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu wa kimataifa ni ishara ya kuwa ushiriki wa Tanzania katika nyanja za uandaaji wa viwango na udhibiti ubora umezidi kuimarika.

“Uwepo wa wageni hao utatoa fursa ya kipekee ya kutangaza bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, jambo ambalo linaweza kusaidia wazalishaji kupata masoko ya kimataifa, kukuza biashara na kuchangia katika maendeleo ya uchumi endelevu wa Taifa letu,” amesema Katunzi.
Ameeleza kuwa mkutano huo utaambatana na maonesho ya bidhaa mbalimbali, na kutoa wito kwa wazalishaji wa ndani pamoja na watoa huduma wakiwemo wa sekta ya utalii kushiriki kikamilifu, kudhamini na kutumia fursa hiyo kutangaza bidhaa na huduma zao.
Kaulimbiu ya mkutano huo ni:“Kuharakisha Haki katika Biashara Ndani ya Eneo la Biashara Huria Barani Afrika (AfCFTA) Kupitia Mifumo Madhubuti na Viwango Vilivyoainishwa.”
Amesema mkutano huu ni fursa muhimu kwa Tanzania kuonyesha maendeleo yake katika sekta ya viwango na ubora, pamoja na kuwezesha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi wanachama wa ARSO.



