Tanzania nafasi ya pili mapambano dhidi ya rushwa

DAR ES SALAAM: Tanzania imeendelea kupiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, hali inayothibitishwa na takwimu za kimataifa zilizotolewa na Taasisi ya Transparency International.

Akizungumza leo katika mjadala Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Tanzania inashika nafasi ya pili kwa nchi za Afrika Mashariki katika juhudi za kupambana na rushwa, ikitanguliwa na Rwanda pekee. katika Bara la Afrika lenye jumla ya nchi 54, Tanzania inashika nafasi ya 14.

“Kwa vipimo vya Transparency International vinavyopima mwenendo wa rushwa duniani, Tanzania ni ya pili kwa Afrika Mashariki. Ndani ya bara la Afrika, tumefikia nafasi ya 14. Hii inaonyesha kuwa tuko kwenye njia sahihi na tumepiga hatua kubwa katika kupambana na rushwa na ufisadi,” amesema Prof. Kitila.

Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akijibu swali la mtangazaji Charles William kuhusu mtazamo wa baadhi ya Watanzania, hasa wa kipato cha chini, wanaoamini kuwa umasikini wao unasababishwa na rushwa na uzembe wa viongozi.

Katika mjadala huo uliobeba mada isemayo “Je, Serikali ya Awamu ya Sita Imeweza Kugusa Maisha ya Watanzania?”, Profesa Kitila amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imejipanga kikamilifu kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vyote vya rushwa.

Ameongeza kuwa kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030, Serikali imejipanga kuimarisha utawala bora kwa kudhibiti rushwa, ufisadi, uzembe na wizi wa mali za umma ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania wote bila ubaguzi.

Prof. Kitila amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kuchukua hatua madhubuti na kuhakikisha kuwa mafanikio yanayopatikana katika vita dhidi ya rushwa yanaendelezwa kwa maslahi mapana ya taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button