Tanzania, Pakistan kushirikiana kibiashara

TANZANIA na Pakistan zimeahidi kuendelea kushirikiana kuimarisha zaidi sekta za biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili.

Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Salvastory Mbilinyi alipokutana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Shehryar Akbar Khan katika majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Pakistan.

Mbilinyi amesema Pakistan ni miongoni mwa nchi za Asia ambazo zina majadiliano ya kidiplomasia na Tanzania.

Advertisement

Amesema chimbuko la majadaliano hayo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Pakistan.

Akizungumza katika mkutano uliokutanisha pande hizo mbili katika opfisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam, Mbilinyi amesema Serikali imejikita zaidi katika kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji nchini hivyo wafanyabiashara kutoka Pakistan wasisite kuwekeza Tanzania salama.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Shehryar Akbar Khan amesema Pakistan na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali wakati wote.

“Nchi zetu zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali, ila kwa sasa tunaona ni vyema zaidi tukaimarisha zaidi sekta ya biashara na uwekezaji kwani kila nchi inahitaji biashara na uwekezaji,” alisema Khan.

Katika mazungumzo hayo pande zote mbili zimeahidi kuimarisha ushirikiano katia sekta za elimu, afya, ulinzi, kilimo, nishati uchumi wa buluu na usafirishaji.