Tanzania ya tatu EAC abiria wa ndege kulipia tiketi kidijiti

DAR ES SALAAM: ABIRIA wa mashirika ya ndege nchini wanaweza sasa kulipia tiketi za ndege kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi baada ya kuzinduliwa kwa huduma mpya ya malipo ya kidijiti .

Huduma hiyo mpya imezunduliwa mwishoni mwa wiki kati ya Shirika la Ndege la flydubai na Kampuni ya Mawasiliano ya Network International na kufungua ukurasa mpya kwa Tanzania kuwa nchi ya tatu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya Kenya na Uganda kunufaika na mfumo huo wa kisasa wa malipo ya simu.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo la mawasiliano la Network International Kanda ya Afrika Mashariki, Judy Waruiru alisema huduma hiyo ya malipo ya kidijiti kupitia simu za mkononi kwa usafiri wa anga ni hatua inayolenga kukuza matumizi ya malipo ya kidijiti na kuimarisha ushirikishwaji wa kifedha katika kanda.

Judy alisema kupitia huduma hiyo, wateja wa shirika hilo la ndege waliopo nchini wanaweza kulipia safari zao moja kwa moja kwa kutumia mitandao mbalimbali ya simu kama Mixx by Yas na Airtel Money, wanapokata tiketi kupitia tovuti au programu ya simu ya shirika hilo.

“Huduma hii inaleta suluhisho mbadala la ndani na lisilotegemea fedha taslimu, kwa wasafiri wengi waliokuwa wakikumbwa na changamoto za malipo ya tiketi kwa njia za kimataifa pekee,’’alisema Judy.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Kitengo cha Uendeshaji Biashara wa flydubai kwa kanda ya Falme za Kiarabu, GCC, Afrika na Asia Kusini, Sudhir Sreedharan alisema ushirikiano wao na kampuni ya Network International unatokana na mafanikio waliyopata katika nchi za Kenya na Uganda.

“Mafanikio tuliyopata katika nchi hizo yameonesha dhamira yetu ya kutoa njia nyingi na rahisi za malipo kwa wateja wetu. Tutaendelea kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya ndani huku tukiboresha huduma zetu kwa wateja kote duniani,”alisema Sreedharan.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button