Tasac yaonya usafirishaji holela

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limewataka wamiliki na wadau wa usafiri wa majini kuepuka usafirshaji holela wa mizigo na abiria katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka kwa maslahi binafsi ili kuepuka ajali.

Ofisa Mfawidhi wa Tasac mkoa wa Geita, Godfrey Chegere ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea mialo ya uvuvi na usafirishaji eneo la Nkome halmashauri ya wilaya ya Geita kwa lengo la kutoa elimu ya usalama majini

Amesema kila chombo cha usafiri wa majini kilichokaguliwa na kuidhinishwa na Tasac kimepewa leseni yake kulingana na muundo na uwezo wake na hivo kubadilishia matumizi ya chombo cha majini huenda ikapelekea ajali.

Advertisement

“Niwasisitize wamiliki wote wa vyombo vya abiria, wasipakie abiria kuzidi uwezo, au wasibadilishe matumizi ya kubadilisha abiria wakapakia abiria, kwani ni kinyume na kanuni zetu za Tasac.

“Wahakikishe wanafuata utaratibu, kama ni chombo cha abiria kipakie abiria, kwa uwezo ambao tumekipatia leseni na kama ni mizigo basi kipakie mizigo, kwa uzito kulingana na leseni”, amesema Chegere.

Amesema Tasac imejidhatiti kuimarisha usimamizi wa vyombo vyote vya majini katika kuangalia usalama na ubora wa vyombo vya maji na kuhakikisha elimu ya matumizi sahihi ya vifaa vya uokoaji.

“Endapo mtu yeyote anayemiliki chjombo cha majini atabainika kuytotumia ‘life jacket’ (Boya Okozi) basi hatutosita kumuchukulia hatua kali za kisheria” amesema.

Aidha amewakumbusha wasafirishaji na wavuvi wanaoenda kufanya shughuli zao katika ziwa Viktoria wahahakikishe kabla ya kuondoka wanapata taarifa za hali ya hewa ili waweze kuwa na uhakika juu ya usalama wao majini.

Msajili wa vyombo vya abiaria mwalo wa darajani Nkome, Japhet Athanas amekiri ukaguzi wa kabla na baada ya kuondoka kwa boti zote imesaidia kila chombo kuzingatia sheria na kanuni za Tasac na kupunguza ajali.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombat amewapongeza Tasac kwa hatua wanazoendelea kuchukua na kuwataka wananchi kuzingatia kanuni na taratibu na kuepuka kuendesha shughuli zao kiholela.