TAWA yapunguza utegemezi serikalini

MOROGORO: MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),imepiga hatua za kimaendeleo na kuiwezesha kupunguza utegemezi kwa serikali kwa asilimia 80 kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika kwa muda mfupi katika nyanja mbalimbali.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo, Meja Jenerali Mstaafu ,Hamis Semfuko amesema hayo makao makuu ya mamlaka hiyo mkoani Morogoro kwenye halfa ya kijeshi ya kuangwa kwa Kamishna wa uhifadhi mstaafu , Mabula Misingwi Nyanda .
Meja Jenerali Mstaafu ,Semfuko amesema kutokana na maboresho makubwa yakiwemo ya kiutendaji, utegemezi kwa Serikali kwa Tawa sasa umebaki ni wa asilimia 20.
Mwenyekiti wa Bodi huyo amesema kwa muda mrefu Bodi pamoja na Menejimeti ilikuwa na jukumu la kuijenga Mamlaka hiyo ikiwemo kubadilisha mifumo na kuingia ya kitaasisi ikiwemo uboreshaji wa maslahi ya watumishi wake.
Amesema kutokana na mabadiliko hayo ,Mamlaka hiyo imekuwa ni miongoni mwa taasisi za uhifadhi zinazikubalika na kuwa imara zaidi.
Meja Jenerali Mstaafu Semfuko amesema chini ya uongozi wa Kamishna Mstaafu Mabula aliwezesha kuleta nidhamu na kazi kubwa ya kuongeza mapato.
“ Wakati anachukua uongozi mapato yalikuwa nduni na kwa kiasi kikubwa Mamlaka ilikuwa ni tegemezi kwa Serikali na anaondoka hali ya mapato ni ya kuridhisha na hadi sasa utegemezi kwa serikali umebaki ni kwa asilimia 20” amesema Mwenyekiti wa Bodi hiyo ,Semfuko.
Amesema jambo hilo limewezekana kutokana na ubunifu mkubwa uliofanyika na Menejimeti ya Tawa chini ya Kamishna aliyestaafu kusimamia kuanzisha mfumo kugawa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada wa kielektroniki.
Pia amesema kuanzisha Mkataba wa Uwekezaji Mahiri kwenye maeneo ya Wanyamapori (Special Wildlife Investment Concession Areas- SWICA) kwa kitalu cha uwindaji katika maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka hiyo na kumewezesha kuleta wateja wengi .
“ Mambo haya muhimu yamewezesha kuleta mabadiliko makubwa katika uhifadhi utalii , uweklezaji, mazingira bora ya utendaji kazi na kuongezeka kwa mapato “ amesema Meja Jenerali Mstaafu Semfuko.
Naye Kamishna Uhifadhi Mstaafu wa Tawa , Mabula Misungwi Nyanda katika hotuba yake ya kuaga ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuipatia fedha Mamlaka hiyo za uendeshaji wakati wote.
Amesema wakati Mamlaka hiyo ilipoanza ilikuwa inaingiza mapato ya Sh bilioni 25.7 na kiwango hicho kilikuwa ni katika mwaka wa fedha 2020/2021.
Nyanda amesema kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa kupitia Bodi ya Wakurugenzi kwa kushirikiana na menejimenti waliweza kuongeza mapato zaidi hadi kufikia zaidi ya Sh bilioni 75 kwa mwaka fedha 2023/2024
Awali kabla ya kumkalibisha Kamishna Uhifadhi Mstaafu, Kaimu Kamishna waTawa ,Mlage Kabange amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana miongozi iliyotolewa na Bodi hiyo yenye viongozi wabobezi katika nyanja mbalimbali na uweledi wao umeiwezesha kuijenga na kuiimalisha Mamlaka hiyo.