TCRA yahimiza umakini, weledi habari za uchaguzi

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imehimiza umakini na weledi kwa waandishi na vyombo vya habari vya utangazaji katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Oktoba 29 mwaka huu.

Meneja Kitengo cha Huduma za Utangazaji wa TCRA, Andrew Kisaka alisema hayo Dar es Salaam jana katika mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Alisema ni vema vyombo vya utangazaji na waandishi kuwa makini wanapochakata habari zao ili Tanzania ivuke salama kwenye uchaguzi mkuu.

“Uzushi hautakiwi, si umesikia uvumi kidogo tu umeshatangaza, tuhakikishe tunabaki kwenye weledi mwanzo mpaka mwisho wa uchaguzi,” alisema Kisaka.

Alisema, vyombo hivyo vinapaswa kufuata sera za vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi kwani kazi ya waandishi ni kufahamisha wananchi sera za vyama ili wananchi wachuje, ndio maana hutakiwi (mwandishi) kutoa maoni yako binafsi,” alisema.

“Tusiingie kwenye kutoa taarifa binafsi za wagombea, tusiingie kwenye ubaguzi wa udini na ukabila…kama unafanya mahojiano wanasiasa hakikisha unayemuhoji ameruhusiwa na chama chake kufanya hivyo,” alisema.

Akizungumzia kuhusu midahalo, Kisaka alisema si ruhusa kufanya mdahalo na chama kimoja: “Kama studio ulialika wagombea watatu kaja mmoja basi hutakiwi kuendelea na mdahalo, lakini wanaweza wakawa wagombea wengi akakosekana mmoja kwenye huo mdahalo basi tunaweza kuendelea nao,” alisema.

Aidha alisema waandishi wajiweke mbali na utangazaji habari wanazoona zinaweza kuvuruga amani ya nchi na hilo linaweza kuepukika.

Tayari vyama vya siasa vipo kwenye mchakato wa kuteua wagombea wao katika nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa Inec, fomu wa wagombea wa nafasi ya rais na makamu wa rais zinatarajiwa kuanza kutolewa Agosti 9-27 na wale wagombea wa nafasi ya ubunge na udiwani fomu zinatarajiwa kuanza kutolewa Agosti 14-27.

Aidha, Agosti 28 mpaka Oktoba 28, itakuwa ni kipindi cha kampeni kwa upande wa Bara na Zanzibar kampeni zitaanza Agosti 28-Oktoba 27.

Jumla ya majimbo 272 yatahusika katika uchaguzi huo, 222 Bara na 50 ya Zanzibar.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button