TCU yaongeza muda udahili, yafungua dirisha awamu ya 3

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imeongeza muda wa kutuma maombi ya udahili na kufungua awamu ya tatu ya dirisha la maombi kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza, waliokosa udalihi katika awamu ya kwanza na ya pili katika mwaka wa masomo 2025/26 utakaoanza Oktoba 6, 2025 hadi Oktoba 10, 2025.

Pia, imesema udahili kwa dirisha la awamu ya pili umekamilika na matokeo yatatangazwa na vyuo ifikapo Oktoba 6, 2025.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa imeeleza kuwa TCU ilipokea maombi ya kuongeza muda wa kutuma maombi ya udahili kutoka kwa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) pamoja na vyuo vya elimu ya juu, kwa ajili ya waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika awamu zilizopita na kwa programu ambazo bado zina nafasi.

Imesema kwa waombaji waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja katika awamu ya pili na wale walioshindwa
kuthibitisha udahili katika awamu ya kwanza wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimoja kuanzia
Oktoba 6, hadi 19, 2025.

Profesa Kihampa amesema wanafunzi hao wanapaswa kufanya udahili kupitia akaunti zao walizotumia kuomba udahili kwa awamu ya pili.

Aidha kwa mujibu wa TCU, imetoa ratiba ya udahili wa awamu ya tatu inayoonesha baada ya kufunga dirisha Oktoba 10, 2025 kuanzia Oktoba 14 hadi 16, 2025 vyuo vinapaswa kuwasilisha majina ya waliodahiliwa katika
awamu hiyo.

Imesema ifikapo Oktoba 20, 2025 vyuo vitatangaza majina ya waliodahiliwa katika awamu ya tatu na kuanzia Oktoba 20 hadi Novemba 3, 2025 itakuwa ni muda wa kuthibitisha udahili kwa waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja katika awamu ya tatu na wale walioshindwa kuthibitisha udahili wao katika awamu zilizopita.

TCU ilisisitiza kuwa kwa waombaji wa udahili wa shahada ya kwanza wanapaswa kujithibitisha katika chuo
kimoja na kwenye chuo husika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button