Mlongazila yaondoa mawe bila upasuaji

DAR-ES-SALAAM : HOSPITALI ya Taifa Muhimbili -Mloganzila iliyopo jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Taasisi ya MediAfric Tanzania imeanza kambi maalum ya kuvunja mawe kwenye njia ya mkojo kwa kutumia teknolojia ya kisasa bila mgonjwa kufanyiwa upasuaji.

Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Mkojo, Dk. Hamis Isaka huduma hiyo itatolewa kwa muda wa siku tano kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 03, 2025 ambapo zaidi ya wagonjwa 12 watahudumiwa. SOMA: Mlongazila kupandikiza meno bandia

“Kufanyika kwa huduma hizi za kuondoa mawe kwenye njia ya mkojo bila kufanya upasuaji, ni hatua kubwa kwani kunadhihirisha namna Serikali ilivyofanya uwekezaji ambao umelenga kupunguza usumbufu na gharama kwa wananchi kwa kuhakikisha huduma hizi zinapatikana katika hospitali za Umma nchini, Mloganzila ikiwemo” amesema Dk. Isaka.

Dk. Isaka amebainisha kuwa wataalam wa hospitali hiyo wataendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, huku wakiweka msisitizo katika kuushauri uongozi kuhusu uanzishwaji wa huduma mbalimbali ambazo zina tija na zinazolenga kuwapunguzia gharama ya kuzitafuta nje ya nchi.

Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila ni miongoni mwa hospitali za Umma hapa nchini ambayo imejikita katika kutoa huduma za ubingwa bobezi. Huduma hizo ni  kupandikiza figo kwa kuvuna figo kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia matundu madogo, kupandikiza nyonga na magoti, kupandikiza uloto, kupunguza uzito kwa kutumia puto maaluma na upasuaji wa matundu madogo.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button