TEMESA yaanza kufanyia kazi malalamiko ya wateja

SIMIYU: Wakala Wa Ufundi na Umeme (TEMESA) imeanza kufanyia kazi malalamiko ya wateja wake, ambao wengi walilalamikia gharama kubwa za matengenezo ya magari, pamoja na matengenezo yasiyofikia viwango.

Malalamiko mengine yalikuwa ucheleweshaji wa matengenezo, uwepo wa mafundi wasiokuwa na uwezo, na uadilifu, uhaba wa vipuli, pamoja na kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha.

Hayo yamesema leo na Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi (TEMESA), Hassan Karonda alipomwakilisha Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo wakati wa kikao cha wadau wa TEMESA Mkoa wa Simiyu.

Karonda amesema kuwa changamoto ya gharama za matengenezo, TEMESA imeingia mkataba na wazabuni zaidi ya 56 kwa ajili ya kutoa huduma ya vipuli pamoja na vilainishi kwa gharama nafuu.

“ Gharama kubwa ambazo wateja wetu walikuwa wanalalamikia asilimia 70 zilitokana na vipuri na vilainishi, katika mkakati wetu mpya tumeingia mkataba na wazalishaji moja kwa moja wa bidhaa hizo ambazo wanatupatia kwa gharama nafuu,” alisema Karonda.

Kuhusu mafundi wasiokuwa na ujuzi, weledi na uadilifu, Mkurugenzi huyo alisema kuwa wameingia mkataba na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya ufundi stadi (VETA) kwa ajili ya kuwapatia mafundi wenye ubora ujuzi wa kutosha.

“ Karakana zetu zote nchi nzima tumefunga kamera ili kukomesha wafanyakazi wasiokuwa na weledi na uadilifu na mpaka sasa zaidi ya watumishi 7 wakiwemo mafundi wamechukulia hatua za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi katika mikoa ya Dodoma na Kigoma,” alieleza Karonda.

Alisema kuwa mbali na hilo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa mwaka huu wa fedha imetoa kiasi cha Sh milioni 700 kwa ajili ya ununuzi wa vitendea kazi lengo likiwa kuboresha utendaji kazi wa taasisi hiyo.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Anna Gidalya alizitaka taasisi zinazodaiwa na TEMESA kuhakikisha zinalipa madeni yao ili taasisi hiyo iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Habari Zifananazo

Back to top button