TET, Soma Kwanza wakubaliana kuboresha elimu

DAR ES SALAAM: TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikiana na wadau kutoka Soma Kwanza wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kuboresha Sekta ya Elimu nchini ili kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora na ya kidijitali.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba amesema malengo ya makubaliano ni kuimarisha na kuendeleza elimu nchini kupitia kuandaa vifaa na miundombinu ya kidigitali itakayosaidia kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji.

Advertisement

Amesema Soma Kwanza wataanzisha televisheni, redio, na programu (apps) kwa jina la TIE – Soma Kwanza Television vitavyosaidia kuchochea ujifunzaji na ufundishaji katika Sekta ya Elimu nchini.

Ameongeza kuwa kwa pamoja watashirikiana kuwezesha upatikanaji wa miundombinu (vifaa, utaalam, na rasilimali fedha), huku TET ikiratibu upatikanaji wa wataalamu wa ufundishaji wa teknolojia za elimu (Educational technologies) katika shule za serikali, mijini na vijijini.

Pia amesema kuwa katika mitaala iliyoboreshwa serikali imeimarisha matumizi ya Tehama na teknolojia nyingine katika ufundishaji na ujifunzaji, hivyo matumizi ya Tehama yamechopekwa  katika  vitendo vya ufundishaji na ujifunzaji katika masomo yote kuanzia ngazi ya elimu ya awali.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu kutoka Soma Kwanza, Peter Kangere amesema, Soma Kwanza itaendelea kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya Elimu kuhakikisha watoto wa Tanzania hawatabaki nyuma katika mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea duniani.

Sambamba na hilo Kangere amesema, maudhui ya elimu yatayokuwa yakitolewa katika televisheni, redio na programu za TIE – Soma Kwanza yatawiana na Mtaala ulioboreshwa ili wanafunzi kutoka pande zote wapate Elimu yenye ubora na kwa njia rahisi.