TFS yafikia asilimia 8.3 ya upandaji miti Silayo

GEITA: WAKALA wa Huduma za Misitu Nchini (TFS) imefanikiwa kupanda miti 6,041,618 katika eneo la hekari 5,438 sawa na asilimia 8.3 ya hekta 65,248.54 za shamba la miti Silayo lililopo wilayani Chato mkoani Geita.
Ofisa Mhifadhi Mwandamizi wa TFS katika Shamba za Miti Silayo, Libenti Elizeus ametoa taarifa hiyo Septemba 07, 2025 mbele ya viongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa 2025 walipotembelea mradi wa chanzo cha mto Mtakuja.
Amesema upandaji wa miti hususani katika chanzo cha maji mto Mtakuja ndani ya Shamba la Miti Silayo katika Kijiji cha Minkoto ni sehemu ya juhudi za kulinda vyanzo vya maji na utunzaji wa mazingira.
Amesema chanzo cha maji cha mto Mtakuja ndani ya shamba la miti Silayo, ni miongoni mwa vyanzo zaidi ya 14 vilivyopo ndani ya shamba hilo la miti na TFS imejidhatiti kulinda vyanzo vyote vya maji.
“Lengo la mradi huu ni kuendelea kutunza vyanzo vya maji, kusaidia utunzaji wa miti, uoteshaji wa miche na kuwasaidia wananchi waliopo kwenye mkondo wa maji.
“Mradi wa chanzo cha maji umegharimu kiasi cha sh milioni 19 kwa ajili ya kuulinda na kuuhifadhi, tangu kufufuliwa kwake mwaka wa fedha 2017/18” amesema.
Amesema wananchi takribani 2,000 wanaozunguka chanzo cha maji Mtakuja wanapata manufaa kwa kupata maji ya matumizi ya kila siku ikiwemo kufulia, kuoga, kunywesha mifugo na kilimo cha umwagiliaji.
Amesema mpango endelevu wa mradi huo ni kupanua uwigo wa uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa kupanda miti Rafiki kando ya vyanzo vya maji sambamba na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi amepongeza hatua hiyo kwa kuwa shughuli ya upandaji miti ndio mpango bora zaidi wa kuendeleza utunzaji wa mazingira asilia.



