Thamani ya sekta ya benki yafikia tril 67/-

SEKTA ya benki inaendelea kufanya vizuri kiasi cha kufikisha thamani ya Sh trilioni 67.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Akaro alisema mbali na benki kufikisha thamani hiyo, pia zimeondoa mikopo chechefu kutoka asilimia 9.9 mwaka 2020 mpaka asilimia 3.3 mwaka 2025.
Akaro aliyasema hayo wakati alipomwakilisha Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba kwenye uzinduzi wa shindano la Taasisi ya Taaluma za Kibenki (TIOB) linaloshirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu.
“Sekta ya kibenki ni imara, tulivu na stahimilivu katika nyanja zote. Kwa miaka minne ama mitano hivi faida imeongezeka mpaka asilimia 25, mitaji ni asilimia 21, kuna ukwasi wa asilimia 30… ndio maana unaona mikopo inayotolewa kwa sekta binafsi ni mikubwa sababu kuna ukwasi wa kutosha na benki zinazidi kuongezeka,” alieleza.
Shindano hilo la TIOB linafanyika kwa mwaka wa pili mfululizo likitarajiwa kushirikisha wanafunzi zaidi ya 2,000 kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Akizungumzia shindano hilo litakaloendeshwa kwa miezi mitatu kuanzia jana mpaka Julai 7, 2025, Akaro alisema ni jambo zuri kwani inahitajika elimu kwa vijana juu ya shughuli za kibenki na utunzaji wa fedha.
“Unakuta kijana msomi kabisa ameingia kwenye kucheza bahati nasibu ili apate fedha, ama anacheza upatu anaambiwa toa Shilingi milioni mbili upate Shilingi milioni kumi, umeona wapi kitu kama hicho. Lazima ujue kama hapa unaibiwa… tuendelee kutoa elimu tusichoke,” alisema Akaro.
Alisema BoT kama mdhibiti mkuu wa sekta ya fedha nchini ina jukumu muhimu la kuhakikisha sekta ya fedha inakuwa na maendeleo endelevu yenye tija na inachangia kwa kiwango kikubwa katika kukuza uchumi.
“Uchumi wa nchi yoyote ikiwa ni pamoja na Tanzania unategemea sana mfumo wa kifedha ulio imara na wenye ufanisi hivyo tunahitaji wataalamu wabunifu katika sekta ya kibenki na fedha ambao watakuwa na ujuzi wa kutatua changamoto zinazojitokeza,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIOB, Patrick Mususa alisema wanatarajia mwaka huu watafikia vyuo vingi zaidi nchini kwenye shindano hilo kulinganisha na mwaka jana.
“Mwaka jana tulikuwa na vyuo 49 na wanafunzi walioshiriki walikuwa 2,460… tuna ushirika mzuri kutoka kwenye sekta za kibenki na wafadhili mbalimbali ikiwemo BoT ambayo ndio mfadhili mkuu,” alisema Mususa.
Alitoa rai kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kujitokeza kushiriki zaidi katika kupata elimu ya fedha kwa vitendo na hilo ni kwa wanafunzi wote wanaopenda kupata elimu ya fedha kwa vitendo si wale wanaosoma masuala ya fedha pekee.
Shindano hilo litafanyika kupitia programu maalumu ya WhatsApp na baada ya mshiriki kujisajili atatakiwa kubuni jina la benki atakayoiendesha, kuunda bidhaa za mikopo ikiwamo kiasi cha mwisho cha kukopesha na kiwango cha riba kwa kila aina ya mkopo, kuunda bidhaa za amana na kiasi cha akiba ya kuanzia na riba ya kila aina ya amana.
“Mshindi atapatikana kwa kupata kiwango cha asilimia cha juu zaidi ya mapato halisi ya riba, kupata uwiano wa kiwango cha fedha za kukidhi malipo ya fedha taslimu juu ya asilimia 70,” alieleza Mususa.
“Kupata uwiano wa mikopo ya jumla ya amana usiozidi asilimia 80, kuhakikisha uwiano wa mikopo chechefu na jumla ya mikopo wa chini ya asilimia tano, kuhakikisha uwiano wa mtaji na jumla ya mikopo wa juu asilimia 10.5,” alisema.



