THBUB yalaani vurugu za uchaguzi mkuu

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imelaani vurugu iliyotokea nchini kipindi cha Uchaguzi Mkuu na kusababisha vifo, uharibifu wa mali na uvunjifu wa amani katika baadhi ya maeneo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini  Dodoma ,Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu alisema matukio hayo hayapaswi kuungwa mkono kwa sababu yanavunja amani katika nchi na kuvunja usalama wa wananchi.

Amesema kutokana na matukio hayo, tume imepanga kufanya uchunguzi wa kina. “Tumekwishajipanga katika jambo hilo ili tuweze kuona ni maeneo yapi ambayo kwa kuangalia matukio yaliyojitokeza tume inaweza kutoa ushauri kwa serikali na vyombo vingine kwa madhumuni ya kutaka kuendelea kulinda amani katika nchi yetu,” alisema. Jaji

Mwaimu amesema matukio yaliyojitokeza yamevunja baadhi ya haki za wananchi kwa sababu wamepoteza maisha na wengine wamepoteza mali. Alisema tume imeona matukio hayo yanapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kina ili waweze kutoa ushauri namna ya kuondokana na matatizo ya namna hiyo miaka mingine ya uchaguzi. “Kwa namna yoyote ile matukio yote hayo hayapaswi kuungwa mkono kwa sababu yanavunja amani katika nchi na usalama kiujumla,” alisema.

Ameongezea kuwa THBUB imewahimiza wananchi kote nchini kuendelea kutunza tunu ya amani kwa kuzingatia misingi ya katiba na kanuni za nchi kwani inapotokea uvunjifu wa amani kila mmoja anashindwa kufanya shughuli zake za kila siku. SOMA: Maadili na haki za binadamu: Mvutano wa aina yake Afrika

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button