THRDC yawanoa watetezi haki za watoto

DODOMA: Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umetoa mafunzo kwa washiriki 40 wanaojihusisha na utetezi wa haki za watoto, yenye lengo la kuwawezesha kuandaa ripoti kivuli kwa mujibu wa sheria, taratibu na mifumo rasmi ya haki za binadamu.
Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi na Mkuu wa Idara ya THRDC, Wakili Paul Kisabo, ambaye amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za mtandao huo kuwawezesha watetezi kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto za haki za watoto, pamoja na kukuza ushiriki wao kwenye mifumo ya haki za binadamu ya kikanda na kimataifa.
“Mafunzo haya ni sehemu ya jitihada endelevu za kuwajengea uwezo watetezi wa haki za watoto ili kuongeza ubora wa ripoti na ushawishi wa utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na taasisi za kimataifa,” alisema Wakili Kisabo.

Amesema, Watetezi wa haki za watoto nchini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa uelewa wa kutosha kuhusu mchakato wa kuandaa ripoti mbadala, ujuzi wa kiufundi, pamoja na ushirikiano mdogo na serikali katika kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa kuhusu haki za watoto.
Kwa mujibu wa Wakili Kisabo, Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda kuhusu haki za watoto, ikiwemo Mkataba wa Haki za Mtoto. Mikataba hiyo inaitaka nchi kuwasilisha taarifa kuhusu hali ya utekelezaji wa haki za watoto kila baada ya miaka minne au mitano.
Aidha, mashirika ya kiraia yanayotetea haki za watoto nayo yanapaswa kuandaa ripoti kivuli zinazowasilishwa katika taasisi za kimataifa, kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na kamati za haki za watoto.
THRDC imesema itaendelea kutoa mafunzo na msaada wa kiufundi kwa wadau mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa uandaaji wa ripoti hizo, na kuhakikisha kuwa sauti za watoto na masuala yao yanazingatiwa katika maamuzi ya kitaifa na kimataifa.



