TLS Iringa yajitosa sakata waliobomolewa nyumba Iringa

IRINGA: CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society – TLS), kupitia ofisi yake ya Kanda ya Iringa, kimeahidi kuchukua hatua baada ya kuzuka kwa madai ya kuvunjwa kwa nyumba za familia kadhaa katika eneo la Don Bosco, mjini Iringa.
Ubomoaji huo unaodaiwa kufanywa na watu waliotajwa kuwa ni madalali, huku taratibu za kisheria zikidaiwa kupuuzwa.
Taarifa na video zilizovuja kwenye mitandao ya kijamii zimeonesha wakazi wakiwa katika majonzi na taharuki, wakieleza kuwa nyumba zao zilibomolewa ghafla, bila notisi wala maelezo kutoka kwa mamlaka yoyote rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mwenyekiti wa TLS Kanda ya Iringa, Wakili Moses Ambindwile, alisema chama hicho kimeanza kufuatilia kwa kina chanzo na uhalali wa ubomoaji huo.
Alisema iwapo itabainika kuwa haki za wakazi hao zimekiukwa, TLS ipo tayari kutoa msaada wa kisheria kupitia Dawati la Msaada wa Kisheria linaloongozwa na Wakili Mchungaji Joshua Chussy.
“Kama TLS, tunalazimika kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi ananyang’anywa haki zake bila kufuata sheria. Kila mtu anastahili kusikilizwa na kupata haki mbele ya sheria kabla ya hatua yoyote kuchukuliwa dhidi yake, ikiwemo kuondolewa katika makazi,” alisema Wakili Ambindwile.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Sheria ya Tanganyika Law Society (The Tanganyika Law Society Act, Cap 307), TLS ina mamlaka ya kushughulikia masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wanaohitaji.
Wakili Ambindwile alibainisha kuwa TLS Kanda ya Iringa ina historia ya kushiriki kikamilifu katika masuala ya utetezi wa haki, akitolea mfano kesi ya mwaka 2024 ambapo TLS ilimsaidia kisheria Maria Ngoda, aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 22 kwa kukutwa na vipande 12 vya nyama ya swala.
Kwa msaada wa TLS, Mahakama Kuu ya Tanzania ilibatilisha hukumu hiyo na kumuachia huru, baada ya kubaini kasoro katika mwenendo wa kesi hiyo.
TLS imewataka wananchi wote waliokumbwa na tukio la ubomoaji au matukio mengine ya ukiukwaji wa haki, kujitokeza na kuwasiliana na dawati la msaada wa kisheria ili hatua za kisheria zichukuliwe ipasavyo.



