TMDA ‘yakomaa’ viwango WHO

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imefanikiwa kushikilia hadhi ya Kiwango cha Tatu cha Ukomavu (WHO Maturity Level 3) wa Mfumo wa Udhibiti wa Dawa na Chanjo, kufuatia tathmini ya kina iliyofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2023.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dk. Adam Fimbo, imesema mamlaka inajivunia hatua hii, ikithibitisha umahiri, uwazi na weledi katika kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za afya. Dkt. Fimbo alisema kuwa Tanzania kupitia TMDA iliweka historia mwaka 2018 kuwa mamlaka ya kwanza barani Afrika kufikia hadhi hii ya WHO Maturity Level 3 (WHOML3).
“Kushikilia hadhi hii baada ya ukaguzi uliofanyika mwaka 2023 ni ishara ya mifumo endelevu ya udhibiti, ikithibitisha uongozi na mchango wake mkubwa katika kulinda afya ya jamii. Hii ni hatua muhimu ikijumuisha ubora, usalama na ufanisi wa dawa na chanjo, ulinzi dhidi ya bidhaa duni au bandia, na uwezo wa kukabiliana na dharura za kiafya kama milipuko ya magonjwa,” amesema Dk. Fimbo.
Aidha, Dk. Fimbo alisema mafanikio haya yanathibitisha jitihada endelevu za TMDA katika kuimarisha mifumo ya udhibiti, kunaifanya Tanzania kuwa kwenye nafasi nzuri kimataifa, ikiwemo ushiriki wa programu za pamoja za udhibiti, fursa za masoko ya kikanda na kimataifa, na kuvutia wawekezaji katika sekta ya dawa na vifaa tiba. TMDA imealika wananchi kusherehekea mafanikio haya kama nchi na inatambua mchango wa washirika wa maendeleo, wadau, wataalamu wa afya, na wananchi kwa ujumla. SOMA: Watanzania kupatiwa huduma za afya kwa simu